Zahanati ya Kanyerere Sengerema yaanza kutoa huduma
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wananchi wa kijiji cha Kanyerere wilayani Sengerema wameishukuru serikali kwa kuhakikisha huduma za afya zinapatikana katika kijiji hicho na kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kupata huduma za afya.
Decemba 26 mwaka jana Pause Tv ililipoti changamoto wanayoipata wakazi wa kijiji cha Kanyerere ya kutopata huduma ya afya licha ya majengo ya zahanati kukamilika.
Kwa kuona changamoto hiyo, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Mohamed Mchengerwa alitoa maagizo kwa viongozi wa mkoa wa Mwanza wahakikishe zahanati ya Kanyerere inaanza kutoa huduma ya afya kwa wananchi na kuwaondolea adha kwa wajawazito na watoto ambao wanalazimika kutembea umbali wa kilometa 15 kufuata huduma za mama na mtoto.
Baada ya maagizo hayo Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw.Balandya Elikana alitoa maagizo ya kupatiwa taarifa kuhusu mchakato wa ukamilishaji wa miradi 17 ya afya wilayani Sengerema iliyojengwa kwa nguvu ya wananchi ili hatua za haraka zifanyike wananchi wapate huduma.
Mwenyekiti wa kijiji hicho cha Kanyerere Charles Kalamu amesema zahanati hiyo ilianza kufanyakazi mara ya aagizo la waziri wa TAMISEMI ambapo viti,meza na vifaa tiba viliwekwa katika zahanati hiyo na halmashauri ya Sengerema kupitia afisa maendeleo ya jamii Yusta Mwambembe iliwapatia wataalamu wa afya wawili.
Kalamu amesema kuwa kwa hivi sasa zahanati hiyo ina Wahudumu wawili na wahudumu wengine watatu wanatoka zahanati ya Buzilasoga na kufanya idadi ya wahudumu kufikia watano.
“Wananchi wamefurahi sana zahanati hii kuanza kufanyakazi hasa kina mama hivi sasa wakishika ujauzito hawana hofu kwa sababu wanaweza kujifungua kwa wakati bila tatizo lolote” alisema Kalamu.
Matilda Mpina mkazi wa kijiji cha Kanyerere anasema wanashukuru Mungu kwa Zahanati hiyo kuanza kufanyakazi ambapo sasa kina mama wajawazito na watoto hawapati usumbufu wa kutembea umbali mrefu ili kuifuata huduma.
“Yaani tunafuraha kubwa sana kwa hivi sasa hata vifo vya kina mama wajawazito vimepungua na magonjwa yanayotokana na kuchelewa kupatiwa huduma ya kujifungua kama fistula yamepungua kwa hivi sasa” alisema Matilda.
Wilaya ya Sengerema ina jumla ya vituo 6 vya kutolea huduma mbalimbali za afya kati ya hivyo vituo vya Afya moja (1) ni Hospital inayomilikiwa na serikali, kituo kwa kushirikiana na taasisi ya dini, zahanati 18 zinazomilikiwa na serikali, zahanati 3 zinazomilikiwa na watu binafsi, zahanati 3 Parastatal na kliniki 1 ni maternity home.
Huduma za afya ya Mama na Mtoto zimeendelea kuimarika wilayani Sengerema Kukiwa na ongezeko la kiwango cha wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya huku wastani wa wanawake wajawazito wanane (8) hadi kumi (10) hujifungua kila siku katika hospitali ya wilaya.
Aidha, vifo vya akinamama wajawazito vimepungua kutoka 11/100,000 mwaka 2014 8/100,000 Disemba 2015, 6/100,000 hadi kufikia Juni 2017 vifo viliripotiwa 3/100,000.
Sambamba na huduma hizo za wajawazito, pia huduma za kuzuia maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto (PMTCT).
Uimarishwaji wa vituo vya afya nchini unakwenda sambamba na lengo la program ya jumuishi ya taifa ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (MMMAM) ambayo ni kutoa huduma jumuishi kwa watoto katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na afya bora.
Imeandaliwa na Tonny Alphonce, Mwanza
No comments: