UWADOMAMI wasaini makubaliano na wenye malori Kwimba
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mwakilishi wa kampuni ya Magdalena Investment, Moshi Kalad (kulia) akisaini makubaliano na umoja wa wafanyabiashara wadogo katika masoko na minada mkoani Mwanza (UWADOMAMI) kwa ajili ya kusafirisha mizigo katika minada wilayani Kwimba.
Makubaliano hayo yameshuhudiwa na Makamu Mwenyekiti wa UWADOMAMI Mkoa Mwanza, Lucas Ponsiano (kushoto), Katibu wa UWADOMAMI Mkoa Mwanza, Davis Philipo (wa pili kushoto) na wanachama wa UWADOMAMI wilayani Kwimba.
Meneja kampuni ya Jilot Investment, Simon Charles akisaini makubalino na UWADOMAMI kwa ajili ya kampuni hiyo kusafirisha mizigo ya wafanyabiashara wadogo kwenye minada wilayani Kwimba.





***
Umoja wa wafanyabiashara wadogo katika masoko na minada mkoani Mwanza, umesaini makubaliano na wamiliki wa malori kwa ajili ya kusafirisha mizigo ya wanachama wake kwenye minada mbalimbali wilayani Kwimba.
Makubaliano hayo yalisainiwa Alhamisi Juli 18, 2024 katika ukumbi wa Ngasamo uliopo Hungumalwa wilayani Kwimba ikiwa ni mwendelezo wa UWADOMAMI kusaini makubaliano na wasafirishaji mizigo kwenye minada mkoani Mwanza.
Makamu Mwenyekiti wa UWADOMAMI mkoani Mwanza, Lucas Ponsiano alisema makubaliano hayo yatasaidia pande zote mbili kufanya kazi kwa weledi huku mizigo ya wafanyabiashara ikiwa salama kwani kampuni itakayofanya uzembe na kupoteza mizigo itawajibika kulipa.
Naye Katibu wa UWADOMAMI Mkoa Mwanza, David Philipo alisema tayari zoezi la umoja huo kusaini makubaliano na wasafirishaji mizigo katika minada limefanyika katika Wilaya za Nyamagana, Ilemela, Magu, Sengerema na Kwimba ambapo Wilaya inayofuata ni Misungwi.
Nao wasafirishaji mizigo waliosaini makubaliano hayo ya miaka minne walisema yatawasaidia kufanya kazi kwa ubora zaidi bila kuingiliwa na mamluki ambao walikuwa wanabeba kinyemera mizigo ya wafanyabiashara katika masoko na minada na inapopotea inakuwa changamoto kuwapata.
PIA>>> BONYEZA HAPA KUSOMA ZAIDI
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
No comments: