LIVE STREAM ADS

Header Ads

Vijana watakiwa kutumia Ndondo kuonyesha vipaji

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mratibu wa mashindano ya mpira wa miguu ya Ndondo Cup, Shafii Dauda amewataka wachezaji kutumia mashindano hayo ili kuonyesha vipaji vyao.

Dauda alisema hayo Juni 30,2024 wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Ndondo Cup 2024 katika uwanja wa Kinesi wilaya ya Ubungo jijini Dar-es-salaam.

Dauda alisema mashindano hayo yameanza na ni wakati sasa vijana kuweza kucheza na kuonyesha vipaji vyao ili waweze kutimiza malengo yao waliojiweka katika mchezo wa soka.

Katika hatua nyingine aliishauri jamii kuhakikisha inafanya mazoezi ili kuwa na afya imara.

"Watu wote katika jamii yetu wanatakiwa kufanya mazoezi ili kuepuka tatizo la magonjwa yasioambukizwa. Pia ili mtu kuwa imara ni lazima awe na utaratibu wa kupima afya" alisema.

Alisema Mashindano ya Ndondo Cup yameshirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya katika kuhamasisha ufanyaji wa mazoezi kupitia kampeni ya Mtu Ni Afya, yenye kauli mbiu ya Fanya kweli, usibaki nyuma.
Dauda alisema kampeni ya Mtu Ni Afya, ni jambo kubwa sana na Wizara inasistiza watu wote wafanye mazoezi.

Naye Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dk Ntuli Kapologwe alisema kilichowavutia Wizara yake kufadhili mashindano ya Ndondo cup ni kuwa mashindano hayo yanaibua vipaji vya vijana.

Akielezea kuhusu kampeni ya Mtu Ni Afya, Dk Ntuli alisema kampeni hiyo imejikita katika michezo na ufanyaji wa mazoezi.

"Michezo ni sehemu ya uimarishaji wa Afya kwa maana inaimarisha kinga pamoja na misuli.Pia Ndondo cup imelenga kuinua vipaji vya vijana katika maeneo mbalimbali" alisema.

Dkt. Ntuli alisema kwa sasa michezo imekuwa sehemu kubwa ya fursa na ajira kwa vijana.Katika hatua nyingine amesema kama Wizara wataendelea kusisitiza ufanyaji wa mazoezi katika jamii.

‘’Msisitizo wetu sisi kama Wizara ni ufanyaji wa mazoezi mara kwa mara ili watu wawe na afya bora na imara’’ alisema.
Naye Mchezaji kutoka timu ya Makuburi, Abdulkarim Kassim alisema mechi yao dhidi ya Manzese Warriors FC ilikuwa ngumu sana na iliyojaa upinzani mkubwa.

‘’Mashindano hayo ni fursa kwetu sisi vijana katika kuonyesha vipaji vyetu, tunaishukuru kamati ya Ndondo Cup na Wizara ya Afya kwa kuona umuhimu wa mashindano’’ alisema.

Alisema kampeni ya Mtu Ni Afya, itasaidia katika kuhamasisha mazoezi kwa wachezaji wanaoshiriki mashindano ya Ndondo Cup pamoja na vijana wengi sehemu mbali mbali.

Katika mchezo wa uzinduzi kati ya Makuburi FC na Manzese Warriors uliisha kwa sare ya bila kufungana. Mchezo huo ulichezwa katika uwanja wa Kinesi wilaya ya Ubungo.

No comments:

Powered by Blogger.