LIVE STREAM ADS

Header Ads

World Vision, KIVULINI wakabidhi vifaa tiba na vitendea kazi Shinyanga

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Shirika la World Vision Tanzania linalotekeleza miradi ya NOURISH na GROW ENRICH mkoani Shinyanga kwa kushirikiana na shirika la KIVULINI, limekabidhi vifaa tiba na vitendea kazi vyenye thamani ya shilingi milioni 159.2.

Vifaa hivyo vimekabidhiwa Julai 24, 2024 kwa Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Anamringi Macha kwa ajili ya kuvikabidhi kwa wakurugenzi wa Halmashauri za Shinyanga Vijijini na Kishapu miradi hiyo inakotekelezwa.

Meneja shirika la World Vision Tanzania Kanda ya Ziwa, Jacqueline Kaihura amesema baadhi ya vifaa tiba vilivyokabidhiwa ni pamoja na mashine za kupima saratani ya mlango wa kizazi kwa akina mama, mizani ya kupimia uzito kwa watoto na akina mama, vifaa vya upasuaji, vitanda na pamoja na projekta za kutolea elimu kwa jamii.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la KIVULINI, Yassin Ally amesema shirika hilo limekabidhi baiskeli 75 kwa ajili ya kurahisisha usafiri kwa watoa huduma za afya ngazi ya jamii kuzifika kaya kwa kaya kutoa elimu ya lishe na afya.

Akipokea vifaa hivyo, Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Anamringi Macha amesisitiza kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Baadhi ya watoa huduma za afya ngazi ya jamii mkoani Shinyanga akiwemo Lucy Cosmas na Venance Ngasa wamekiri kuwa awali walikuwa na changamoto ya usafiri.

Mradi wa NOURISH unaofadhiliwa na nchi ya Ujerumani unatekelezwa Kishapu huku mradi wa GROW ENRICH unaofadhiliwa na IRELAND ukitekelezwa Kishapu na Shinyanga Vijiji ambapo miradi yote miwili ni ya miaka mitano kuanzia 2023/27 ikilenga kuimarisha lishe bora, afya ya mama na mtoto na afya ya uzazi wa mpango kwa vijana balehe.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Anamringi Macha.
Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Anamringi Macha akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi vifaa tiba na vitendea kazi mkoani Shinyanga vilivyotolewa na shirika la World Vision Tanzania na shirika la KIVULINI.
Meneja shirika la World Vision Tanzania Kanda ya Ziwa, Jacqueline Kaihura.
Mkurugenzi Mtendaji shirika la KIVULINI, Yassin Ally akizungumza kwenye hafla hiyo.
Baadhi ya watoa huduma za afya ngazi ya jamii mkoani Shinyanga wakiwa kwenye hafla hiyo.
Meneja shirika la World Vision Tanzania Kanda ya Ziwa, Jacqueline Kaihura (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Anamringi Macha vifaa tiba.
Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Anamringi Macha akiendesha baiskeli baada ya kupokea baiskeli 75 zenye thamani ya shilingi milioni 16.8 zilizotolewa na shirika la KIVULINI kwa ajili ya watoa huduma wa afya ngazi ya jamii katika wilaya za Shinyanga na Kishapu.
Baiskeli zilizotolewa na shirika la KIVULINI kwa ufadhili wa shirika la World Vision Tanzania.
Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Anamringi Macha (wa nne kuoka kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa afya mkoani humo.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.