LIVE STREAM ADS

Header Ads

Viongozi kutoka Zanzibar wahitimisha ziara ya kimafunzo Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar imepongeza mchango wa shirika la kutetea haki za wanawake na watoto KIVULINI katika kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Abeida Rashid Abdallah ametoa pongezi hizo Julai 05, 2024 jijini Mwanza wakati wa hitimisho ya ziara ya siku tatu ya kujifunza mbinu ya SASA inayotumiwa na shirika hilo kutoa elimu ya kupambana na ukatili wa kijinsia.

Kufuatia kazi kubwa iliyofanywa na shirika la KIVULINI katika kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii ikiwemo kupinga ukatili wa kijinsia, Abdallah aliahidi kuwa Wizara yake itashirikiana na shirika hili na taasisi nyingine katika kuimarisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia visiwani Zanzibar.

Akizungumza na wadau mbalimbali wanaojihusisha na mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani Mwanza, Abdalah aliziasa taasisi nyingine kufika Mwanza ili kujifunza namna mbinu ya SASA inavyosaidia kutokomeza ukatili wa kijinsia.

Pia alibainisha dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuelekeza nguvu zaidi katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwenye ngazi za chini ili kuleta matokeo chanya tofauti na sasa ambapo mapambano hayo yanafanyika kwenye ngazi ya kitaifa pekee.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIULINI, Yassin Ally alishukuru uongozi wa Wizara ya Maendeleo ya Mamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar kufanya ziara ya mafunzo jijini mwanza na kujifunza mbinu zinazotumiwa na shirika hilo kufikisha elimu kwa jamii.

Ally aliahidi kuwa shirika la KIVULINI liko tayari kuendelea kutoa uzoefu wake kwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuhakikisha wanasaidia mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kwa watoto na wanawake na kwamba shirika hilo liko tayari kufungua ofisi visiwani Zanzibar.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Abeida Rashid Abdallah.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Abeida Rashid Abdallah (kulia) akizungumza na Afisa Mnazimu wa jeshi la polisi mkoani Mwanza wakati wa ziara ya kujifunza kuhusu mbinu za kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia zinazotumiwa na Dawati la Jinsia na Watoto.
Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar wakiwa katika ofisi za jeshi la polisi mkoani Mwanza kujifunza mbinu za kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar wakiwa na viongozi wa dini mkoani Mwanza kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu za kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI, Yassin Ally akizungumza na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar walipokutana na viongozi wa dini mkoani Mwanza.
Sheikh wa Mkoa Mwanza ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mwanza, Hassan Kabeke akitoa uzoefu namna viongozi wa dini walivyosaidia kutoa elimu ya kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.
Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa Mwanza, Mchungaji Dkt. Jacob Mutashi akitoa uzoefu namna viongozi wa dini walivyosaidia kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia mkoani Mwanza.
Mmoja wa Wanamabadiliko mkoani Mwanza ambaye ana uoni hafifu akitoa uzoefu namna watu wenye ulemavu wanashiriki katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa dini mkoani Mwanza na wafanyakazi wa shirika la KIVULINI.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.