LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wananchi wahimizwa kuchangamkia fursa za uwekezaji kwenye mapori

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeshiriki maonesho ya 48 ya kimataifa ya kibiashara yanayoendelea jijini Dar es Salaam ili kuhamasisha umma wa watanzania wawekezaji na wageni kutoka mataifa mbalimbali kuwekeza katika maeneo inayoyasimamia huku ikijinasibu kuwa na fursa lukuki za uwekezaji.

Akiongea na wageni waliotembelea banda la TAWA lililopo ndani ya banda la Wizara ya Maliasili na Utalii Afisa Utalii, Daud Tesha alisema TAWA ina uwanda mpana wa fursa za uwekezaji unaotoa mwanya kwa wawekezaji wa aina mbalimbali kuwekeza katika Taasisi hiyo.

Akizitaja fursa hizo, Tesha alisema yapo maeneo mengi yanayohitaji wawekezaji na uwekezaji katika Taasisi hiyo kama vile maeneo ya utalii wa picha kwenye maeneo ya hifadhi za Wanyamapori, maeneo ya kihistoria yenye Utalii wa kiutamaduni, eneo la uwekezaji mahiri (Special Wildlife Investment Concession Areas - SWICA), uwindaji wa kitalii na ufugaji wa wanyamapori.

"TAWA imetenga maeneo kadhaa kwa ajili ya kufanyika shughuli za utalii wa picha kutokana na ikolojia na aina ya vivutio vilivyopo katika maeneo hayo ikiwemo pori la akiba Mpanga/ Kipengere eneo ambalo lina maporomoko ya maji zaidi ya 10 ambayo hutoa burudani safi kwa watalii" alisema Tesha.

"Maeneo mengine ni pori la akiba Wamimbiki, Tabora Zoo, Ruhila Zoo , Makuyuni Wildlife Park ambapo wananchi wanakaribishwa kuwekeza kwenye miundombinu ya utalii ikiwemo kujenga kambi za kulala wageni, hosteli, loji na maeneo ya mapumziko mafupi kwa watalii (picnic sites)" alisema Tesha.

Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi kutembelea banda la TAWA ili kupata maelezo ya fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika taasisi hiyo.

"Kama kauli mbiu ya Maonesho haya inavyosema kuwa Tanzania ni mahali sahihi pa biashara na uwekezaji, nitumie fursa hii kuwaambia watanzania wote kuwa TAWA ni taasisi sahihi kwa biashara na uwekezaji kwani inatoa fursa za uwekezaji wa aina mbalimbali" alisema Maganja.

Maonesho hayo yalianza Juni 28, 2024 na yanatarajiwa kufikia tamati Julai 14, 2024.
Na Beatus Maganja, Dar es Salaam

No comments:

Powered by Blogger.