SHEREHE ZA MWAKA MPYA ZAWALETA PAMOJA WANANCHI NA MHANDISI JUMBE
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mdau wa Maendeleo Mhandisi, James Jumbe, leo Januari Mosi, amekutana na makundi mbalimbali ya wananchi wa Manispaa ya Shinyanga katika hafla ya pamoja ya kuukaribisha Mwaka Mpya 2026, iliyofanyika nyumbani kwake, Mtaa wa Majengo, Kata ya Kambarage.
Hafla hiyo ya chakula cha pamoja, iliyojaa furaha, upendo na mshikamano, ni sehemu ya utamaduni wake wa kila mwaka wa kutumia nyakati za sikukuu kukutana na wananchi, kuzungumza nao ana kwa ana na kuimarisha mahusiano ya kijamii.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhandisi Jumbe amesema kuwa mshikamano, upendo na ushirikiano kati ya wananchi ndiyo nguzo muhimu za kuimarisha maisha ya kijamii.
Mhandisi, James Jumbe akipata chakula
“Sikukuu zina thamani zaidi pale tunapokaa pamoja, kula pamoja na kutambua kuwa maisha hayaishi kwa mtu mmoja bali kwa jamii nzima. Jamii imara hujengwa kwa upendo, mshikamano na kugusana kimaisha,” amesema Jumbe.
Ameeleza kuwa ataendelea kudumisha utamaduni huo kila mwaka kama njia ya kuimarisha ukaribu, maelewano na mshikamano miongoni mwa wananchi, huku akihamasisha jamii kujali na kuthamini makundi mbalimbali.
Wananchi walioshiriki katika Sherehe hizo za kuukaribisha Mwaka Mpya 2026 ,wamempongeza Mhandisi Jumbe kwa moyo wake wa kujitoa, wakisema kuwa ni mtu anayeishi maisha ya kawaida ya wananchi na anayejali mahusiano ya kijamii kwa vitendo.
Hivi karibuni, kabla ya kufanyika kwa hafla ya chakula cha pamoja cha kuukaribisha Mwaka Mpya, Mhandisi Jumbe alitembelea Kituo cha Wazee Kolandoto pamoja na Shinyanga Society Orphanage Centre, ambako alikabidhi zawadi na vyakula vya sikukuu kwa wazee na watoto wanaolelewa katika vituo hivyo, ikiwa ni ishara ya kujali, kushiriki furaha ya sikukuu na kugusa maisha ya makundi yenye uhitaji.































No comments: