Taasisi ya PFC yasaida miradi ya maendeleo Busega, Simiyu
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Shirika linalojihusisha na utoaji elimu ya uhifadhi wa wanyamapori la Peace For Conservation (PFC) kupitia mradi wa Lamadi Wash Project, limefanikiwa kujenga vyoo vya kisasa kwa ajili ya wasichana katika shule nne zilizopo Wilaya ya Busega mkoani Simiyu.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo la PFC, David Kabambo ameyasema hayo Agosti 26, 2024 wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali inayofadhiliwa na shirika hilo wilayani Busega.
Kabambo alisema katika mradi wa WASH, shirika la PFC limekamilisha ujenzi wa vyoo katika shule mbili za Antony Mtaka Sekondari na Shule ya Msingi Kijereshi huku ujenzi ukiendelea katika shule za Sekondari Lamadi na Mkula.
"Baada ya miradi hiyo kukamilika, pia tutajenga vyoo katika shule za Sekondari Kijeleshi na Mwabasami ambapo lengo ni kusaidia kupunguza utoro kwa wanafunzi wa kike wanapokuwa kwenye hedhi maana vyoo hivyo vina miundombinu yote muhimu ikiwemo maji, chumba cha kuoga na kubadilishia pedi" alisema Kabambo.
Kando ya ujenzi wa vyoo, Kabambo pia alisema shirika la PFC kwa kushirikiana na wananchi limesaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Sekondari Lamadi na Shule ya Msingi Kijereshi.
"Wasichana sasa watatulia shuleni muda wote na kuzingatia masomo hasa wakati wa hedhi tofauti na awali ambapo mwanafunzi alilazimika kurudi nyumbani na hivyo kukosa masomo. Nitoe shukurani kwa wafadhili wa mradi huu wa ujenzi wa vyoo vya kisasa kwa ajili ya wasichana" alisema mwanafunzi wa Lamadi Sekondari, Eliada Charles.
Naye Teleza Masalu kutoka shule ya Sekondari Mkula alisema vyoo hivyo vinafaa kwa matumizi ya wanafunzi wa kike wakati wa hedhi kwa sababu vina eneo maalumu la kubadilishia pedi na kuhifadhia zilizotumika kwa ajili ya kuteketezwa na hivyo kukidhi mahitaji yao tofauti na vyoo vinavyotumika na wanafunzi wote shuleni hapo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kijereshi, Mashauri Mashimba alisema ushirikiano wa shirika la PFC na wananchi kutoka vijiji vitano vinavyozunguka pori la akiba la Kijereshi ni mkubwa katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu.
"Tunashukuru Mkurugenzi ametuahidi mifuko ya simenti kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Kijereshi, pia shirika la PFC lilitusaidia vifaa vya kujikinga na tembo kama vile tochi, filimbi na mavuvuzera kwa ajili ya kufukuza tembo wasiharibu mazao yetu shambani" alisema Mashimba.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa shirika la Rettet die Elefanten Afrikas (Save the Elephants of Africa) kutoka Ujerumani, Thomas Toepfer kutoka nchini Ujerumani alieleza kufurahishwa na miradi ya kijamii inayotekelezwa na shirika la PFC ikiwemo mradi wa WASH na ulinzi wa tembo katika pori la Kijereshi na kuahidi kuendelea kushirikiana na shirika hilo katika kusaidia utekelezaji wa miradi yake.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mkurugenzi wa shirika la PFC, David Kabambo (kushoto) akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea shughuli zinazofanywa na shirika hilo katika maeneo yanayozunguka pori la wanyamapori Kijereshi. Kulia ni Mwenyekiti wa shirika la Rettet die Elefanten Afrikas (Save the Elephants of Africa) kutoka Ujerumani, Thomas Toepfer ambapo shirika hilo limekuwa likishirikiana na shirika la PFC kwenye utekelezaji wa miradi yake wilayani Busega.
Mwenyekiti wa shirika la Rettet die Elefanten Afrikas (Save the Elephants of Africa) kutoka Ujerumani, Thomas Toepfer akielezea utayari wa shirika hilo kuendelea kushirikiana na shirika la PFC katika ulinzi wa tembo hasa kutokomeza ujangiri katika pori la Kijereshi.
Mhifadhi Daraja la Kwanza, Claudia Shemhina ambaye ni Kaimu Mhifadhi Kamanda Pori la Akiba Kijereshi akieleza namna shirika la PCF linavyoshirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kudhibiti matukio ya ujangiri hasa kwa tembo katika pori hilo.
Picha ya pamoja na wafanyakazi wa Pori la Akiba Kijereshi lililopo Lamadi wilayani Busega.
Picha ya pamoja na wafanyakazi wa Pori la Akiba Kijereshi lililopo Lamadi wilayani Busega.
Shirika la PFC pia lilikabidhi mashine mbili za kusaga nafaka kwa vikundi vya wananchi ambapo miongoni mwa walionufaika na mashine hizo ni kikundi cha wanawake cha Amani Mwabayanda.
Shirika la PFC limekamilisha ujenzi wa choo cha kisasa cha wanafunzi katika shule ya msingi Kijereshi.
Shirika la PFC limekamilisha ujenzi wa choo cha waalimu katika shule ya msingi Kijereshi.
Picha ya pamoja na Kamati ya Maendeleo ya Kijiji cha Kijereshi ambapo shirika la PFC limesaidia ujenzi wa vyoo na vyumba vya madaras.
Shirika la PFC linaendelea na ujenzi wa vyoo kwa ajili ya wanafunzi wa kike katika shule ya sekondari Mkula na hapa waalimu na wanafunzi wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa ziara ya kukagua ujenzi huo.
Shirika la PFC linaendelea na ujenzi wa vyoo kwa ajili ya wanafunzi wa kike katika shule ya sekondari Lamadi na hapa wanafunzi wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa ziara ya kukagua ujenzi huo.
PIA>>> Bonyeza hapa kusoma zaidi
No comments: