Taasisi za Serikali zapigwa msasa
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkurugenzi Mkazi wa Amref Tanzania, Dkt. Florence Temu akizungumza kwenye Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali jijini Dodoma, Septemba 4 2024.
Mkurugenzi Mkazi wa Amref Tanzania, Dkt. Florence Temu akizungumza kwenye Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali jijini Dodoma, Septemba 4 2024.
Shirika la Amref Health Africa Tanzania limeshiriki katika Kongamano la Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 2024, linalofanyika kuanzia tarehe 4 hadi 6 Septemba 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, Dodoma.
Kongamano hilo lenye kauli mbiu, “MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI NI WADAU MUHIMU, WASHIRIKISHWE KUIMARISHA UTAWALA BORA” linakusudia kuleta pamoja wadau wa sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali ili kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika uwanja huu muhimu.
Katika kongamano hilo, Amref Tanzania imetoa mada juu ya uzoefu wake katika nyanja muhimu za usimamizi wa miradi, ufuatiliaji na tathmini ambapo washiriki kutoka mashirika mbalimbali (hasa mashirika madogo, mashirika mapya) walipata fursa ya kujifunza.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mkurugenzi Mkazi wa Amref Tanzania, Dk Florence Temu amewaasa wadau na washiriki kutoka Asasi za kiraia kuandika maandiko ya miradi yenye kuleta tija kwa jamii.
“Ndugu zangu kuna baadhi ya wenzetu wengine tumekuwa tukikosa miradi kutokana na maandiko kutokueleweka na yasiyo na tija kwenye jamii,”amesema.
Baadhi ya mada zilizoangaziwa kwenye kongamano hilo ni pamoja na;
1. Uelewa Kuhusu Usimamizi wa Miradi: Amref Tanzania ilielezea uzoefu wake wa kina katika jinsi ya kusimamia miradi kwa ufanisi, ikiwa ni pamoja na mikakati na mbinu zinazotumika ili kuhakikisha kuwa miradi inatekelezwa kwa kufuata malengo yaliyowekwa.
2. Ushiriki wa Miradi na Uandishi Maandiko Dhana ya Miradi: Umuhimu wa maandiko ya dhana ya miradi katika kupata ufadhili, na jinsi ya kuandaa maandiko haya kwa ubora wa hali ya juu ili kuvutia wadhamini.
3. Uandishi wa Taarifa ya Mfadhili: Amref Tanzania ilitoa mwanga juu ya namna bora ya kuandika taarifa za wazi na za kina kwa wafadhili, ili kudumisha uwazi na kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu.
4. Ufuatiliaji na Tathmini: Amref Tanzania ilielezea mbinu bora za ufuatiliaji na tathmini za miradi, ikiwa ni pamoja na jinsi ya kutumia data na taarifa kwa ufanisi ili kuboresha matokeo ya miradi.
Ushiriki wa Amref Tanzania katika kongamano hili ni sehemu ya jitihada zake za kuendeleza ushirikiano na wadau katika kuboresha utekelezaji wa miradi na kuongeza ufanisi katika sekta ya afya na maendeleo.
No comments: