LIVE STREAM ADS

Header Ads

DC Nyamagana ahamasisha wananchi kutunza mazingira

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Nyamaga mkoani Mwanza, Amina Makilagi akipanda mti kwenye eneo la chanzo cha maji Butimba ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha wananchi kupanda miti na kutunza mazingira.

Na Hellen Mtereko, Mwanza
Miche ya aina mbalimbali zaidi ya elfu tatu ambayo ni rafiki katika vyanzo vya maji, imepandwa kwenye chanzo cha maji Butimba jijini Mwanza ili kusaidia uhifadhi wa mazingira na kulinda chanzo hicho.

Hayo yamebainishwa Jumanne Octoba Mosi 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi wakati akizungumza kwenye zoezi la upandaji miti katika chanzo hicho lililojumuisha wadau mbalimbali.

Makilagi alisema ni vyema kila mmoja katika jamii kuwa kielelezo katika utunzaji wa mazingira kwa kulinda na kuitunza miti inayopandwa katika taasisi za umma na kuhakikisha haiharibiwi hasa na mifugo.

"Tumepanda miti kwenye chanzo cha maji na mwenge wa uhuru utakapofika kwenye Wilaya yetu ya Nyamagana utakagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na upandaji wa miti hivyo zoezi tulilolifanya leo tumetekeleza kauli mbiu ya mbio za mwenge 2024 ambayo inasema "Tunza mMazingira, Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu" alisema Makilagi.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Maliasili na Mazingira Jiji la Mwanza, David Joseph alisema upandaji wa miti unasaidia kuhifadhi mazingira hususani katika kupunguza hewa ya ukaa.

Naye Afisa Uhifadhi Mwandamizi kutoka Wakala wa Huduma za Mistu (TFS) Wilaya ya Nyamagana, Emmanuel Mgimwa alitoa rai kwa wananchi kuendelea kupanda miti katika maeneo yao ili kuendeleza utunzaji wa mazingira.

Alisema kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025 wanatarajia kutoa bure zaidi ya miche laki tatu kwa jamii ikiwemo ya matunda, kimvuli na urembo.

"Miti hii tutakayoitoa inatakiwa kutunzwa ili thamani ya pesa ya Serikali inayotumika kugharamia miche hiyo iweze kuonekana" alitoa rai Mgimwa.
Afisa Uhifadhi Mwandamizi kutoka Wakala wa Mistu Wilaya ya Nyamagana, Emmanuel Mgimwa akipanda mti katika eneo la chanzo cha maji Butimba.
Mwanamuziki H. Baba akipanda mti kwenye chanzo cha maji Butimba.
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Butimba wakishiriki zoezi la upandaji wa miti katika chanzo cha maji Butimba.
Kaimu Afisa Maliasili na Mazingira Jiji la Mwanza, David Joseph akizungumza wakati wa zoezi la kupanda miti katika chanzo cha maji Butimba.

No comments:

Powered by Blogger.