Dadas Rise wakabidhi taulo za kike wilayani Misungwi
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Zaidi ya wanafunzi 80 wa kike katika shule ya sekondari Mwambola iliyopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, wamekaidhiwa taulo za kike (pedi) ili kuwanusuru na changamoto ya kushindwa kuhudhuria masomo wakati wa hedhi.
Akizungumza Ijumaa Oktoba 18, 2024 baada ya kupokea msaada huo uliotolewa na umoja wa wakurugenzi wa mashirika yanayoongozwa na wanawake vijana mkoani Mwanza (Dadas Rise), Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mwl. Joseph Bujiku alieleza kuwa ukosefu wa taulo za kike unachangia kwa kiasi kikubwa watoto kuwa watoro.
"Mtoto anapopata hedhi akiwa shuleni anashindwa kujistiri hivyo analazimika kurudi nyumbani na wengine wanaamua kukaa kabisa hadi hedhi iishe ndipo aanze kuja shule, hiyo ukosefu wa taulo za kike unachochea utoro na unawafanya watoto washindwe kujiamini" alisema Mwl. Bujiku.
Kwa upande wake Afisa Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Mwl. Dayana Kuboja alisema baadhi ya familia hazina uwezo wa kuwanunulia watoto wao taulo za kike hivyo amewaomba wadau na mashirika mbalimbali kuendelea upatikanaji wa taulo hizo.
Naye Mariam Samweli ambaye ni mmoja wa wanafunzi walionufaika na msaada huo alisema utawasaidia kujistri na kuachana na nyenzo nyingine kama vitambaa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Teens Corridor, Sophia Nshushi alisema wametoa msaada huo ili kuhamasisha wanafunzi wa kike kusoma katika mazingira salama hususani wanapokuwa kwenye kipindi cha hedhi.
"Pamoja na msaada huu, pia tumewapa elimu ya uongozi kuanzia ngazi ya shule na baadae katika ngazi ya Serikali za Mitaa" alisema Nshushi.
Pia Nshushi alitumia fursa hiyo kuishukuru taasisi ya The Desk and Chair kwa kuwawezesha badhi ya taulo za kike ambazo wamezitoa kwa wanafunzi wa kike shuleni hapo.
Mwakilishi kutoka Shirika la Hope for Youth Development, Anitha Samson alisema wataendelea kutoa elimu ya hedhi salama kwa wanafunzi ili waweze kuwa na uelewa mpana wa suala hilo.
"Taulo za kike zinawasaidia wasichana kuwa na utulivu pindi wanapokuwa kwenye hedhi hivyo tunatoa rai kwa jamii na wadau mbalimbali kuendelea kutuunga mkono katika kuwasaidia wanafunzi wa kike kutimiza ndoto yao kielimu" alisema Mkurrugenzi wa Shirika la Naweza Tena, Esther Morris.
Hafla ya kukabidhi taulo za kike na kutoa elimu kuhusu masuala ya hedhi katika shule ya Mwambola wilayani Misungwi imeanyika ikiwa sehemu ya kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike Duniani ambayo huadhimishwa Oktoba 11 kila mwaka.
Na Hellen Mtereko, Misungwi
Baadhi ya wanafunzi wa kike katika shule ya sekondari Mwambola wilayani Misungwi wakiwa kwenye picha ya pamoja na umoja wa 'Dadas Rise'.
Umoja wa mashirika yanayoongozwa na wanawake vijana (Dadas Rise) mkoani Mwanza wakiwa katika shule ya sekondari Mwambola kwa ajili ya kukabidhi taulo za kike.
Wanachama wa 'Dadas Rise' wakiwa na Afisa elimu Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Mwl. Dayana Kuboja (katikati).
Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari Mwambola, Mwl. Joseph Bujiku akigawa taulo za kike kwa wanafunzi zilizotolewa na Dadas Rise.
Wanachama wa Dadas Rise wakiwa katika shile ya sekondari Mwambola kwa ajili ya kukabidhi taulo za kike.
No comments: