Kamati ya Lishe Jiji la Mwanza yasisitiza wazazi kuchangia chakula kwa wanafunzi
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Kamati ya lishe ngazi ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza imeazimia kuendelea na zoezi la kuoa elimu kwa wazazi na walezi ili kutambua umuhimu wa kuchangia upatikanaji wa chakula kwa ajili ya wanafunzi mashuleni.
Hayo yamejiri Jumatano Oktoba 23, 2024 kwenye kikao cha kamati hiyo kilicholenga kujadili taarifa za utekelezaji wa mpango wa lishe katika kipindi cha robo ya kwanza mwaka wa fedha 2024/2025.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Afisa Lishe Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Emma Kilimali alisema wazazi na walezi wakielimishwa vizuri wataweza kuchangia chakula mashuleni hatua itakayosaidia watoto kufanya vizuri pia kwenye masomo yao.
"Kuna umuhimu mkubwa wa watoto kupata chakula wanapokuwa shuleni kwani mtoto akishinda bila kula anaweza asifanye vizuri kwenye masomo yake, hivyo tunapaswa tujikite katika kutoa elimu ili wazazi waone umuhimu wa kuchangia chakula kwa ajili ya watoto wao" alisema Kilimali.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Jiji la Mwanza, Zena Kapama alisema pamoja na kutoa elimu kwa wazazi ya kuchangia chakula shuleni, pia watafanya uchunguzi wa kila shule ina uhitaji wa chakula kiasi gani kwa kila muhula wa masomo ili mzazi apewe utaratibu wa kuchangia.
"Wazazi watakapopewa utaratibu wa kuchangia fedha kwaajili ya chakula kwa mhula mzima itasaidia kupunguza changamoto ya kutoa fedha kila siku" alisema Kapama.
Naye Afisa Elimu Vifaa na Takwimu, Mwl. Mageni Misambo alisema walimu wakuu wanatamani kuboresha namna ya kupata chakula mashuleni lakini malalamiko yanakuwa ni mengi kutoka kwa wazazi yakiwemo ya kuchangishwa fedha hivyo anaamini elimu hiyo itasaidia kuondoa malalamiko hayo.
Awali akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Mwanza- Kiomoni Kibamba, Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Jiji hilo, Erick Mvati alisema wazazi wanapaswa kuelewa kuwa chakula anachokula mwanafunzi shuleni ni kile kile ambacho angekula nyumbani hivyo ni vyema wakachangia upatikanaji wa chakula kwa ajili ya watoto wao badala ya kudhani wanapoteza fedha zao kutoa michangao yao.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Halmashauri ya Jiji la Mwanza Erick Mvati akifungua kikao cha Kamati ya Lishe ngazi ya Halmashauri kilicholenga kujadili taarifa za utekelezaji kipindi cha robo ya kwanza mwaka wa fedha 2024/2025.
Wajumbe wa Kamati ya Lishe ngazi ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza wakiwa kwenye kikao cha kujadili taarifa ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/25.
PIA>>> BONYEZA HAPA KUSOMA ZAIDI
No comments: