LIVE STREAM ADS

Header Ads

RAIS SAMIA: Ghoroma kuanguka Kariakoo ni somo kwetu

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema tukio la kuanguka jengo la ghorofa nne katika Mtaa wa Mchikichi na Manyema uliopo Kariakoo jijini Dar es Salaam, limetoa somo kwa Serikali kuanza uchunguzi wa kuhakikisha kunakuwa na usalama wa binadamu na mali zao kwenye maghorofa yaliyojengwa Kariakoo.

Rais alisema hayo Kariakoo jijini Dar es Salaam, mara baada ya kulitembelea jengo hilo lililoanguka Novemba 16, 2024 na kupewa taarifa kuwa jengo hilo limesababisha vifo vya watu 20.

“Tukio hili limetupa somo kubwa la kuangalia usalama wa majengo yetu katika eneo la Kariakoo, wakati naonyeshwa jengo na nilipoliangalia namna lilivyojengwa kuta zake na nondo zilizotumika bila shaka halikuwa na usimamizi mzuri".

Rais Dkt. Samia aliainisha kuwa ni dhahiri fedha kidogo ndio iliyotumika kujenga jengo hilo kubwa la ghorofa nne bila kujali madhara yatakayotokea kutokana na jengo hilo kutokuwa imara.

“Wakati nikiwa nje ya nchi nilimuelekeza Waziri Mkuu kuunda timu ya uchunguzi na ameniarifu kuwa tayari imeundwa timu hiyo ya watu 20 ambayo inasubiri maelekezo rasmi ya Serikali ianze uchunguzi wa maghorofa yaliyojengwa Kariakoo" alisema.

Pia Rais Dkt. Samia alisema wakati zoezi la kusafisha eneo hilo likiendelea kuna ulazima kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuendelea kufukua kifusi ili kama kuna miili iliyosalia chini itolewe na ipate heshima ya kusitiriwa.

Aidha aliwashukuru wananchi wote waliofika katika eneo la maafa na kujielekeza katika kuwaokoa wahanga badala ya kutaka kuiba ili kujinufaisha na mali zilizopo katika jengo hilo.
Pia, ameelekeza, mali zote zilizopo katika jengo hilo ziende kuhifadhiwa mahali mpaka zoezi la uokozi na usafishaji wa eneo hilo ukamilike, ndio wafanyabiashara waende mahali hapo kutambua mali zao na kuzichukua na hatimaye kuendelea na shughuli za kujiingizia kipato.

Rais Dkt. Samia alitembelea jengo la ghorofa nne lilioanguka Kariakoo jijini Dar es Salaam, baada ya kurejea nchini akitokea Brazil alipoenda kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Kundi la G20 kwa mwaliko wa Rais wa Brazil, Luiz Lula da Silva.
#KaziInaongea

No comments:

Powered by Blogger.