LIVE STREAM ADS

Header Ads

Nyamagana waadhimisha Uhuru wa Tanganyika kwa kupanda miti

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza imeadhimisha sherehe za maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara), Disemba 09,2024 kwa kupanda miche ya miti aina mbalimbali zaidi ya 500.

Ni baada ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt, Samia Suluhu Hassani kutoa agizo fedha zote zilizotengwa Kwa ajili ya maadhimisho ya uhuru zitumike katika kufanya shughuli za kijamii, ikiwemo upandaji miti, kufanya usafi wa mazingira katika maeneo ya kijamii, utoaji wa misaada katika Kambi za wazee pamoja na wahitaji maalum.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amesema katika kuadhimisha siku hiyo wamepanda miti katika shule mpya ya msingi Shadi inayojengwa Kata ya Luchelele, shule ya msingi Buhongwa, Bulale Sekondari na Hospital ya Wilaya ya Nyamagana, Butumba.

Makilagi ameeleeza kuwa upandaji wa miti utasaidia kupata mvua za kutosha, kupunguza mfuriko, kusaidia kukabiliana na ukame pamoja na kupunguza hewa chafu ya ukaa.

"Tusipopanda miti katika Wilaya yetu ya Nyamagana, tutakumbwa na ukame na mvua hazinyeshi au wakati mwingine zinakuwa chache. Lakini pia mvua zinapokuwa chache hatupati chakula" alisema Makilagi.

Naye Askari Mhifadhi Mwandamizi kutoka Wakala Huduma za Mistu Wilaya ya Nyamagana (TFS), Mahija Mkomwa amesema katika kuazimisha sherehe za miaka 63 ya uhuru wa Tanganyika, wamepanda miti zaidi ya 500 katika shule mpya ya shadi iliyopo Kata ya Luchelele.

Kwa upande wake Afisa Mazingira Jiji la Mwanza, David Joseph amesema Taifa limeweka mpango wa kila Wilaya kupanda miti milioni 1.5 ambapo Halmashauri hiyo imeweka mkakati wa kupanda miti elfu sita kila mwaka katika maeneo mbalimbali ya umma.

"Suala la kuhifadhi na kutunza mazingira siyo la Mkurugenzi, sio la TFS, wala siyo la viongozi ni swala shirikishi kwa jamii nzima hivyo jamii lazima itambue namna bora ya kuhifadhi na kutunza mazingira Kwa ajili ya naendeleo yajayo" alisema Joseph.

Mkuu wa shule ya msingi Luchelele ambaye pia ni msimamizi wa shule mpya Shadi, Mwl. Amani Anyosistye ametoa pongezi kwa wananchi kushirikiana na viongozi wa Serikali kupanda miti katika shule hiyo kwa manufaa ya wanafunzi.
Muonekano wa moja ya vyumba vya madarasa katika shule mpya ya Shadi.

No comments:

Powered by Blogger.