Biteko ahimiza upendo ndani ya CCM
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewahimiza viongozi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kupendana, kuvumiliana na kushirikiana ili kuchochea maendeleo kwa wananchi.
Dkt. Biteko ameyasema hayo Jumanne Februari 25, 2025 wakati akizungumza kwenye Mkutano Maalum wa chama hicho jimbo la Msalala, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga ambao umelenga pia kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani kwa kipindi cha mwaka 2020/2025.
“Pendaneni, shikamaneni, jengeni Wilaya yenu, jengeni Halmashauri yenu maana Mungu amewapa kila aina ya utajiri. Katika maisha usigombane na mtu kwa sababu kuna wakati utamhitaji. Hiki chama kimewaleta pamoja, msiruhusu mipasuko miongoni mwenu” amesema Dkt. Biteko.
Aidha Dkt. Biteko pia amewakumbusha wana CCM kusimama imara kumuombea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyeidhishwa hivi karibuni kuwa mgombea urais wa chama hicho kwani ana dhamira kubwa ya kusogeza maendeleo kwa watanzania na kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma bora.
Katika mkutano huo, wana Msalala wakiongozwa na mbunge wao, Idd Kassim wamesema hawana deni na Dkt. Samia hivyo wamejipanga kuhakikisha wanampigia kura za kishindo kwenye Uchaguzi Mkuu 2025 ili kumpa nafasi nyingine ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Tazama BMG TV hapa chini
No comments: