LIVE STREAM ADS

Header Ads

Kamati ya Usalama yasisitiza kasi utekelezaji miradi ya maendeleo

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mwonekano wa vyumba viwili vinavyoendelea kujenga katika Shule ya Sekondari Stanslaus Mabula jijini Mwanza.

Na Hellen Mtereko, Mwanza
Kamati ya Usalama Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza imewataka wasimamizi wa ujenzi shule ya sekondari Stanslaus Mabula kuongeza kasi ili majengo hayo yakamilike kwa wakati.

Rai hiyo ilitolewa Ijumaa February 14, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa katika wilaya hiyo.

Alisema shule ya Sekondari Stanslaus Mabula inatarajia kupanua wigo wa utolewaji elimu kwa kuanza kwa masomo ya kidato cha tano na sita Julai mwaka huu hivyo ni vyema miundombinu hiyo ikakamilika kwa wakati ili wanafunzi wanapofika waanze masomo bila kuchelewa.

"Dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kuwapunguzia adha watoto wanaosafiri mwendo mrefu kwaajili ya kuitafuta elimu katika mikoa mbalimbali hivyo shule hii imechaguliwa mahususi kwaajili ya kuwasaidia watoto kupata elimu karibu hatua itakayosaidia kutimiza ndoto zao" alisema Makilagi.

Aidha alisema pamoja na kuongeza kasi ya ujenzi pia aliwasisitiza kuzingatia viwango bora vya ujenzi ili majengo yawe imara na yaendane na thamani ya fedha iliyotolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.

Mwisho aliwaomba walimu wafanye kazi kwakuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizoweka ili waweze kuwafundisha watoto vizuri hatua itakayosaidia kuwa na elimu bora.

Akitoa taarifa ya ujenzi huo Mkuu wa shule ya Sekondari Stanslaus Mabula, Mwl. Nicholaus Omolo alisema hadi sasa ujenzi huo umetekelezwa kwa asilimia 75.

Alisema shule hiyo ilipokea shilingi milioni 581 Juni 26, 2024 kutoka Serikali Kuu kupitia mradi wa SEQUIP kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne, matundu kumi ya vyoo, mabweni mawili na nyumba mbili za walimu.

Alisema mradi huo utasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi kwa shule jirani ikiwemo Fumagira Sekondari sanjari na kusogeza huduma ya elimu karibu na jamii.
Muonekano wa jengo la bweni linalojengwa Shule ya Sekondari Stanslaus Mabula jijini Mwanza.
Kamati ya Usalama Wilaya ya Nyamagana ikikagua miradi ya elimu jijini Mwanza.

No comments:

Powered by Blogger.