Kamati ya Usalama Nyamagana yakagua miradi ya maendeleo
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi akiwa ameambatana na wajumbe wa Kamati ya Usalama katika ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa shule ya Sekondari Pamba.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Kamati ya Usalama Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza imetembelea na kukagua miradi ya sekta ya elimu katika Kata za Lwanhima, Luchelele na Pamba.
Ziara hiyo ya siku mbili imeanza Alhamisi Februari 13, 2025 ikiwa na lengo la kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa wilayani humo.
Kamati hiyo imetembelea mradi wa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa kwa mfumo wa ghorofa shule ya sekondari Pamba,ujenzi vyumba nane vya madarasa shule ya sekondari Lwanhima, shule mpya za msingi Shadi na kisoko.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Amina Makilagi aliwapongeza wasimamizi wa miradi hiyo kwausimamizi mzuri wa fedha huku akisisitiza miradi hiyo ikamilike kwa wakati ili iweze kuwa na tija kwa jamii.
"Niwapongeze kwa namna mnavyosimamia miradi hii thamani ya fedha inaoneka na miradi ni mizuri endeleeni kuwa waadilifu katika kusimamia fedha za umma kwani hatutamfumbia macho mtu yoyote atakae shindwa kuwa muadilifu katika kusimamia fedha za miradi" alisema Makilagi.
Alisema Serikali inaendelea kutoa fedha nyingi kwaajili ya kuboresha sekta ya elimu hivyo ni vema miradi hiyo ikakamilika kwa wakati ili iweze kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi shule mpya ya msingi Shadi Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Luchelele, Aman Aron alisema ujenzi huo umefikia asilimia 95 na unatarajiwa kukamilika February 25 mwaka huu.
"Shule ya msingi Luchelele ilipokea zaidi ya milioni 300 kwaajili ya ujenzi wa shule ya mkondo mmoja ambayo itawapunguzia watoto mwendo wa kwenda kuitafuta elimu" alisema Mwalimu Aron.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya sekondari Sahwa, Lata Mayombya alisema ujenzi wa shule hiyo umefikia asilimia 98 na kazi zinazoendelea ni kufunga umeme hatua ya pili,kurekebisha sehemu chache zenye dosari,ufungaji wa milango pamoja na matengenezo ya meza 400.
Nao baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Shadi waliishukuru Serikali kwa kuwaletea mradi huo ambao utakuwa mkombozi kwa watoto wao.
"Watoto wetu walikuwa wanatembea umbali mrefu na wengine walikuwa wanaishia njiani hawafiki shule, na baadhi yao walishindwa kumaliza elimu ya msingi lakini kwa sasa watasoma na tunaamini watafanya vizuri kwenye masomo yao" walisema.
Muonekano wa baadhi ya vyumba vya madarasa ya shule ya msingi Shadi.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi akisaini kitabu baada ya kuwasili shule ya sekondari Pamba.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi akiwaongoza wajumbe wa Kamati ya Usalama kukagua mradi wa ujenzi wa shule ya msingi Shadi.
No comments: