LIVE STREAM ADS

Header Ads

Biteko awahimiza watanzania kulilinda Taifa kwa wivu mkubwa

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa watanzania kuendelea kuiombea nchi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

“Tuendelee kuliombea kanisa, tuendelee kuiombea nchi yetu na Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambae kwa kweli anafanya kazi nzuri na sisi tunaofanya kazi karibu naye tunaona” alisema Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko alisema hayo Jumapili Februari 16, 2025 aliposhiriki ibada katika Kanisa la Africa Inland Church Chang’ombe jijini Dar es salaam.

Aliwahimiza Watanzania kudumisha upendo na amani nyakati zote hususan kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, ili uchaguzi huo usiwe sababu ya kuligawa Taifa kutokana na tofauti ya mitazamo.
 
Alisisitiza kuwa “Mungu ametupa bahati ya kuwa na nchi yenye amani, sisi tuilinde kwa wivu mkubwa kwa kuwa amani ikiondoka gharama yake ni kubwa. Tuziombee pia nchi jirani zenye matatizo kwa vile tatizo la jirani linaweza kuwa tatizo lako wakati wowote ule, mfano mnakumbuka janga la covid 19 lilivyotuathiri dunia nzima”.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko alisema Serikali imeendelea kuboresha mipango na sera mbalimbali ili kuendana na mahitaji ya dunia, ametolea mfano mabadiliko yaliyofanyika katika Sera ya Elimu.

“Tunatengeneza Dira ya Taifa ya Maendeleo ambayo tulizunguka nchi nzima kwa ajili ya kukusanya maoni ya watu katika makundi mbalimbali ili tuweze kupata Tanzania tunayoitaka miaka 25 ijayo” alibainisha Dkt. Biteko. 
Akihuburi wakati wa ibada hiyo, Mchungaji Dkt. Joseph Mayala Mitinje aliwaasa waumini wa Kanisa hilo kukumbuka kufanya maombi na kusema kuwa ibada hiyo ilikuwa maalum kwa ajili kuiombea Serikali pamoja na mahitaji mbalimbali.

“Ili umtumie Mungu vizuri una mahitaji ya kila eneo hivyo asubuhi ya leo tunaombea mahitaji yetu kwa Bwana” alisema Mchungaji Mitinje.

Naye Mchungaji Andrew Chad kutoka nchini Uingereza akihubiri katika ibada hiyo, alisema makanisa ya Uingereza na Tanzania yamekuwa na ushirikiano wa karibu na hivyo imeendelea kumpa fursa ya kuhubiri injili nchini.

Alieleza kuwa alipokuja nchini alianza kuhubiri injili katika Kanisa la AICT Mpanda mkoani Rukwa kwa muda wa miaka nane. Baadaye yeye na wenzake walianzisha makanisa mengi katika maeneo mbalimbali ikiwemo mkoani Tanga ambapo alihudumu kwa muda wa miaka sita.

“Tulipata wito kwenda mkoani Tanga kuhubiri injili kwa upande wa watu wa kabila la Wadigo na kuwafundisha watu wanampenda Mungu” alisema Mchungaji Chad.

Aliongeza kuwa Mungu anaweza kumtumia binadamu yeyote kwa utukufu wake, sambamba na kuwaasa wakristu kuishi kwa upendo na kuwa wakarimu kwa watu mbalimbali.

No comments:

Powered by Blogger.