LIVE STREAM ADS

Header Ads

Uwekezaji katika makuzi ya awali ya mtoto watajwa kuwa nguzo ya maendeleo endelevu ya Taifa

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuwekeza katika hatua za awali za malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto, ikitaja hatua hiyo kama msingi imara wa kujenga jamii yenye afya, uelewa na uwezo wa kuchangia maendeleo ya Taifa kwa ufanisi.

Hayo yamebainishwa Jumatano Mei 21, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, kwenye kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM).

Mtanda alisema kuwa hatua ya kwanza ya maisha ya mtoto, kuanzia kuzaliwa hadi miaka minane, ndiyo inayoamua mwelekeo wa maisha yake ya baadaye, na hivyo inahitaji uangalizi wa karibu, lishe bora, mazingira salama na malezi yenye mwitikio chanya.

“Tusipoweka msingi thabiti kwa watoto wetu leo, tutakuwa tunalijengea Taifa mustakabali usio imara. Taifa imara linatokana na watu imara, na watu hao hujengwa tangu awali,” alisema Mtanda.

Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 zinaonesha kuwa zaidi ya robo ya Watanzania ni watoto wenye umri wa kati ya miaka 0 hadi 8, na hivyo kuweka dhahiri haja ya kuwekeza kwa makundi hayo mapema ili kuhakikisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa vizazi vijavyo.

Kwa mujibu wa Mtanda, asilimia 47 ya watoto wa miezi 24 hadi 59 wanaonyesha dalili za ukuaji timilifu wa kiafya na kihisia, jambo linaloonesha umuhimu wa kuendeleza juhudi katika sekta ya afya, lishe, ulinzi na ujifunzaji wa awali.

Craie Ferla, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Children in Crossfire, alieleza kuwa mafanikio yaliyopatikana hadi sasa ni matokeo ya ushirikiano kati ya serikali, taasisi za kiraia na jamii kwa ujumla. Alisisitiza kuwa ajenda ya makuzi ya mtoto si ya muda mfupi, bali ni uwekezaji wa muda mrefu kwa ustawi wa Taifa.

"Watoto wetu si mustakabali wa familia pekee, bali ni nguzo ya maendeleo ya Taifa. Kuwekeza kwao leo ni kuandaa viongozi na wataalamu wa kesho” alisema Ferla.

Khadija Muwango, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka mkoa wa Manyara, alieleza kuwa mafanikio yameonekana tangu kuanzishwa kwa programu hiyo, hasa katika kuboresha huduma za lishe, afya, na malezi ya awali, kupitia kampeni za elimu na ushirikishwaji wa jamii.

Naye Innocent Rusomyo kutoka Shirika la SDO, alisema kuwa ushirikiano na vyombo vya habari na mamlaka za serikali umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uelewa wa jamii juu ya umuhimu wa makuzi ya awali.

Programu Jumuishi ya Taifa ya MMMAM inaendelea kuwa jukwaa muhimu la kushirikisha jamii na wadau wote katika kuhakikisha kuwa kila mtoto wa Kitanzania anapata nafasi ya kukua katika mazingira bora, hali ambayo itajenga kizazi chenye afya, maarifa na uwezo wa kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa.
Na Chausiku Said, Mwanza
Mkuu wa Mkoa Mwanza, Said Mtanda akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau malimbali walioshiriki kwenye kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM).
wadau malimbali walioshiriki kwenye kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM).

No comments:

Powered by Blogger.