Serikali kununua mitambo ya kisasa ili kukabiliana na magugu maji Ziwa Victoria
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Serikali inatarajia kununua mitambo ya kisasa ya kutokomeza magugu yanayotishia shughuli mbalimbali ikiwemo usafirishaji, uvuvu na upatikanaji wa maji katika Ziwa Victoria.
Hayo yamebainishwa Jumamosi Mei 10, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda wakati akizungumza na wananchi katika eneo la Kigongo- Busisi muda mfupi baada ya kushuhudia zoezi la uondoaji magugu maji yaliyotanda katika eneo hilo.
"Leo nimekuja kushiriki zoezi la uondoaji wa magugu maji haya, ukiangalia upande wa pili wa daraja kuna msitu mrefu wa magugu hayo, hii ni hatari kwani maji haya tunayatumia kwa ufugaji wa samaki, usafiri na uendeshaji wa maisha yetu ya kila siku" alisema Mtanda.
Mtanda alisema utaratibu wa ununuzi wa mitambo ya kisasa ili kukabiliana na magugu maji hayo umeshaanza kufanyika na muda si mrefu mitambo mitatu italetwa katika eneo la Kigongo- Busisi kwa ajili ya kuanza kazi ya kusafisha Ziwa.
"Feli zetu tatu zilishindwa kufanya kazi ipasavyo kutokana na magugu maji, kwa sasa tunatumia gharama kubwa hadi milioni mbili kwa siku kwa ajili ya kuwatumia wavuvi wa eneo hili kuyavua ili vivuko visiweze kupata changamoto na wananchi waweze kusafiri vizuri ambapo hadi sasa tumevuna tani 600 za magugu maji" alisema Mtanda.
Aidha Mtanda aliongeza kuwa suala la changamoto ya usafiri katika eneo hilo inakwenda kuwa historia kutokana na daraja la JP Magufuli kukamilika kwa asilimia 99 na hivi karibuni litaanza kutumika baada ya marekebisho ya kingo za barabara kukamilika.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhandisi Cyprian Luhemeja alisema kuna magugu maji ya aina mbili kwa sasa katika Ziwa Victoria ambayo ni mapya na yale ya zamani.
"Hadi sasa yale mapya angalau yameweza kudhibitiwa ila changamoto ipo kwenye yale ya zamani ambayo tutaanza na hatua ya kwanza ya kuyakata ili kuyapunguzia sipidi ya kukua na hatua ya pili Waziri Mkuu alituelekeza tununue mashine za kisasa ili tuweze kuyaondoa kabisa" alisema Mhandisi Luhemeja.
Na Hellen Mtereko, Mwanza



Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akizungumza na baadhi ya wakazi wa Kigongo- Busisi pamoja na abiria waliokuwa wakisubiri usafiri wa kivuko/ feri katika eneo hilo.
No comments: