LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wataalam SADC wakutana Zimbabwe kujadili sekta ya Nishati na Maji

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wataalam wa Wizara ya Nishati pamoja na taasisi zake leo wameshiriki katika Mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu na Watalaam wanaoshughulikia masuala ya Nishati na Maji unaofanyika katika Jiji la Harare nchini Zimbabwe.

Mkutano huo wa awali ni sehemu ya maandalizi kuelekea katika Mkutano wa pamoja wa Kamati ya Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Nishati na Maji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Mkutano huo pamoja na kujadili masuala ya Nishati na Maji, umekuwa ni fursa pia kwa Tanzania kuendeleza diplomasia ya kiuchumi pamoja na kuwasilisha mafanikio ya nchi katika kuboresha huduma za nishati vijijini kupitia miradi inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijjni (REA).

Aidha Mkutano huo umeangazia maendeleo ya Sekta ndogo ya Mafuta na Gesi, pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kikanda ya Mafuta na gesi inayohusu nchi wanachama wa SADC.

Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na taasisi zake waliohudhuria mkutano huo ni Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme, Mhandisi Styden Rwebangila, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mha. Hassan Saidy, Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji (TPDC), Derick Moshi, Mkurugenzi wa Mifumo ya Udhibiti Umeme (TANESCO), Mhandisi Deogratius Mariwa, Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi (EWURA), Msafiri Mtepa na Wataalam kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

No comments:

Powered by Blogger.