LIVE STREAM ADS

Header Ads

Shirika la EMEDO latoa tahadhari watu kuzama majini, kuzuia vifo

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Shirika la usimamizi wa mazingira na maendeleo EMEDO la jijini Mwanza, limetahadharisha kwamba vifo vitokanavyo na watu kuzama maji vinaweza kuzuilika ikiwa hatua za usalama zitachukuliwa mapema.

Meneja mradi wa kuzuia kuzama maji Ziwa Victoria unaotekelezwa na shirika hilo, Arthur Mugema ameyasema hayo wakati wa warsha ya kuwajengea uelewa waandishi wa habari jijini Mwanza kuhusu mradi huo.

Mugema amesema tafiti zinaonyesha kwamba watu wanaofanya shughuli za kiuchumi majini wakiwemo wavuvi, wako kwenye hatari zaidi ya kuzama maji hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari kama kuvaa mavazi okozi (life jackects), kutoingia majini wakiwa wamelewa na kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa kabla ya kuingia majini ambapo shirika hilo limeanza kuweka mabango yenye taarifa hizo katika visiwa vya Ziwa Victoria ikiwemo Goziba.

Naye Afisa Uchechemuzi shirika la EMEDO, Mary Francis amesema lengo la kuwajengea uelewa waandishi wa habari ni kuwaandaa kuwa mabalozi wazuri wa kusaidia kuelimisha jamii kuchukua tahadhari za kujiokoa majini hatua itakayosaidia kukabiliana na vifo vitokanavyo na watu kuzama maji.

Wanahabari vinara wa mazingira jijini Mwanza walioshiriki mafunzo hayo akiwemo Vitus Audax wameweka mikakati ya pamoja ya kushirikiana na shirika la EMEDO kuandaa vipindi na makala mbalimbali za kuelimisha jamii kuchukua tahadhari hatua itakayosaidia kukabiliana na vifo vitokanavyo na kuzama maji.

Itakumbukwa Umoja wa Mataifa uliidhinisha Julai 25 kila mwaka kuwa siku ya kuzuia kuzama maji duniani, ambapo kwa mwaka huu maadhimisho hayo yataambatana na kaulimbiu isemajo, kuzama maji kunazuilika, chukua tahadhari.
Meneja Mradi wa Kuzuia Kuzama Maji Ziwa Victoria unaotekelezwa na Shirika la EMEDO, Arthur Mugema akizungumza kwenye warsha ya kuwajengea uelewa wanahabari jijini Mwanza kuhusu utekelezaji wa mradi huo ulioanza mwaka 2022/2025.
Afisa Uchechemuzi Shirika la EMEDO, Mary Francis akiwasilisha mada kwenye warsha hiyo. 
Wanahabari vinara wa mazingira jijini Mwanza wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa EMEDO.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.