Maonesho ya kwanza ya keki kufanyika Mwanza
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Kwa mara ya kwanza katika historia, wananchi Kanda ya Ziwa.watashuhudia maonesho ya kipekee ya keki yatayofanyika kwa siku tano kuanzia tarehe 03- 07 Septemba katika ukumbi wa 'Gandhi Hall' jijini Mwanza.
Maonesho hayo yatahusisha waoka keki, wapamba keki, waandaa keki na wauza vifaa vya keki.
Moja kati ya waandaaji wa maonesho hayo yaitwayo 'Lake Zone Cake Exhibition', Magdalena Laizer amewahimiza wananchi kujitokeza kushuhudia maonesho hayo ili kujifunza masuala mbalimbali yahusuyo mapishi ya keki.
"Wananchi waje kwa wingi, kwanza waonje keki, wanunue, wajifunze kuhusu sekta hiyo. Pia wakutane na wadau wa keki Kanda ya Ziwa" Laizer.
Kuhusu kiingilio kwa wananchi katika ukumbi wa Gandhi Hall, Magdalena amesema hakuna kiingilio.
Tayari washiriki wa sekta ya keki wamejiorodhesha kwa wingi kushiriki maonesho hayo ya kihistoria
"Idadi ya washiriki inapanda kila siku, hii inatokana na faida watakazopata ikiwa ni pamoja na mafunzo, kuuza bidhaa, kuonjesha keki, kupata tuzo, vyeti, na kubadilishana uzoefu kwa kukutana na wateja wao ana kwa ana" amesema na kuongeza;
"Tunawaomba wadhamini waendelee jitokeze kudhamini maonesho haya ya kipekee ambayo hayajawahi fanyika nchini ili wakuze biashara zao, kujitangaza, kuuza bidhaa, huduma, kukuza alama za biashara na kuifikia jamii kwa urahisi" amebainisha Laizer.
Washiriki wa maonesho hayo ambao ni waoka keki, wapamba keki, waandaa keki, wauza vifaa na wadau mbalimbali katika sekta ya keki watalipia ada ya shilingi 100,000 kabla ya tarehe 20 Agosti 2025 ili kushiriki maonesho hayo.
Maonesho hayo yamedhaminiwa na Helvetas Tanzania, Star TV, RFA, Kiss FM, BJ Empire na Cheza Kidansi ambapo yatakujia mubashara kupitia BMG Online TV.
No comments: