LIVE STREAM ADS

Header Ads

MAVUNDE: TUTAHAKIKISHA WAZAWA WANASHIRIKISHWA KWENYE MGODI MPYA WA NYANZAGA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Madini, Antony Mavunde akizungumza kwenye hafla ya utiaji Saini makubaliano ya nyongeza kati ya Serikali na kampuni ya Nyanzaga Mining Company Limited kwa ajili ya uchimbaji mkubwa wa madini ya dhahabu kupitia kampuni ya ubia ya Sotta .
***

Na Hellen Mtereko, Mwanza
Waziri wa Madini, Antony Mavunde amesema Serikali itahakikisha ushirikishwaji wa wazawa unakuwa wa asilimia kubwa na wananufaika na mradi wa uchimbaji wa dhahabu kupitia kampuni ya ubia ya Sotta Mining Corporation Limited katika mgodi mpya wa Nyanzaga uliopo Sengerema mkoani Mwanza.

Mavunde ameyasema hayo Agosti 20, 2025 wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano ya nyongeza kati ya Serikali na kampuni ya Nyanzaga Miningi Company Limited iliyoko katika Kijiji cha Sotta Kata ya Igalula Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza kwa ajili ya uchimbaji mkubwa wa madini ya dhahabu kupitia kampuni ya ubia ya Sotta Mining Corporation Limited.

Amesema mradi huo wenye zaidi ya shilingi Trilioni moja utakuwa na manufaa makubwa siyo tu kwa wananchi wa Sengerema na mkoa wa Mwanza bali kwa taifa kwa ujumla kwani utatoa ajira za kutosha na ushiriki wa watanzania kwenye kutoa huduma sanjari na uuzaji wa bidhaa mbalimbali.

"Kama Wizara ya Madini tusimamia suala hili vizuri ili wazawa waweze kupata kipaumbele katika mradi huu,pia mmliki wa leseni anawajibu wa kushirikiana na jamii husika hivyo wananchi mliopo katika eneo hili mnakazi ya kuibua miradi yenu nakuipendekeza kwa kampuni ili iwe sehemu ya kampuni kurudisha kwa jamii" amesema Mavunde.

Aidha ameeleza kuwa mchango wa sekta ya madini kwenye pato la taifa uliwekewa malengo ambapo malengo hayo yaliwekwa na Dira ya Taifa, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Sera ya Madini ya mwaka 2009.

"Malengo hayo yalisema kwamba ifikapo mwaka 2025 sekta ya madini ichangie kwa asilimia 10 kwenye pato la taifa lakini kabla ya kufika mwaka huo kwamujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika la Takwimu la Taifa (NBS), sekta ya madini kwa mwaka 2024 imechangia kwenye Pato la taifa kwa asilimia 10.1 kwakipindi Cha mwaka mmoja kabla ya muda uliopangwa" amesema Mavunde.

Amesema maduhuli yaliyokusanywa kwenye sekta ya madini kwa mwaka 2015/2016 yalikuwa ni bilioni 162 kwa mwaka mzima na makusanyo hayo yameendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka ambapo Juni 30, 2025 sekta ya madini wameingiza kwa mara ya kwanza Trilioni 1.7 sawa na asilimia 113 ya lengo lililowekwa.

Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema Sheria inataka Serikali iwe na hisa walau kiwango cha chini asilimia 16 na katika mgodi huo kiwango cha umiliki wa Serikali ni asilimia 20.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema mradi huo utasaidia kuinua uchumi wa mwanza na utasaidia kuongeza uchangiaji wa uchumi wa nchi kutoka asilimia 7.5 hadi kufikia asilimia 10.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa kampuni ya Perseus nchini Tanzania, Lee Anne de Bruin ameishukuru Serikali kwa namna inavyowapa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao huku akiaidi kuendelea kutekeleza makubaliano yote waliyoyasaini kwenye mikataba kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi.

Nao Salome Selemani na Jonathan Mashaka ambao ni miongoni mwa wazawa katika eneo la mradi huo wameeleza matamanio yao ya kupata ajira ili waweze kujiinua kiuchumi.

"Tunatamani sana sisi wazawa tuweze kupata ajira katika mradi huu ili tuweze kusaidia familia zetu,tusomeshe watoto na kujiendeleza kiuchumi" amesema Mashaka.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda. 
Mkurugenzi kampuni ya Perseus nchini Tanzania, Lee Anne de Bruin akizungumza kwenye hafla hiyo.
Baadhi ya wananchi walioshiriki hafla hiyo.

No comments:

Powered by Blogger.