LIVE STREAM ADS

Header Ads

SERIKALI YAREJESHA TABASAMU KWA CHID BENZ: AWAASA WASANII KUKAA MBALI NA DAWA ZA KULEVYA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

 

SERIKALI ya Awamu ya Sita kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kumtibu bure rapa wa muziki wa hip hop nchini, Rashidi Abdallah Mohamed Makwiro (Chid Benz) ambaye kwa miaka kadhaa alitumbukia kwenye uraibu wa dawa za kulevya, hivyo kudhoofika kiafya na kushindwa kutekeleza majukumu yake.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema,Chid Benz ni miongoni mwa Watanzania milioni moja ambao wamepatiwa matibabu bure kutokana na uraibu wa dawa za kulevya kote nchini.

Ameyasema hayo leo Agosti 22,2025 katika ofisi za DCEA jijini Dar es Salaam wakati akimkabidhi Chid Benz kwa familia na Watanzania baada ya Serikali kumpatia matibabu yaliyodumu ndani ya mwaka mmoja.

Ameeleza kuwa, DCEA licha ya majukumu iliyokasimiwa na Serikali ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini, pia imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kunakuwa na ustawi bora wa jamii nchini.

"Lakini, jukumu letu lingine ni kuhakikisha kwamba tunajenga ustawi wa jamii ili wale ambao wamekwishajingiza katika matumizi ya dawa za kulevya tunahakikisha kwamba, tunawaondoa kwenye hayo matumizi ya dawa za kulevya."

Amesema kuwa, mafanikio hayo ya kumpatia Chid Benz na watu wengine matibabu yanatokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ikiwemo miundombinu kwa mamlaka hiyo ili kuhakikisha wale ambao wameathiriwa na dawa za kulevya hususani vijana wanawapatia matibabu nchini.

Serikali inafanya jitihada hizo kwa kutambua kuwa, vijana ni nguvu kazi ya Taifa, hivyo inapaswa kulinda na kusimamiwa kikamilifu ili ilete matokeo chanya katika uchumi na tija kwa Taifa.

Pia, amesema Serikali ina jukumu la kuhakikisha inatibu watu kupitia vituo vya Mat Clinics na kupitia nyumba za upataji nafuu ili kuhakikisha ustawi wa jamii unaendelea kuimarika nchini.

"Ni ili kuhakikisha ustawi wa jamii unaendelea kuimarika na nchi inasonga mbele, na isiyokuwa na watumiaji wa dawa za kulevya. Chid Benz alijikuta ameingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya, lakini baada ya DCEA kufanya operesheni kali ambazo zimesababisha dawa za kulevya kuadimika nchini, aliamua kuanza kutumia dawa tiba zenye asili ya kulevya kama mbadala.

Aidha, Kamishna Jenerali amesema, kutokana na Chid Benz kutokuwa na uelewa kuhusu athari za dawa tiba hizo ambazo zinatumika kwa uangalizi maalum kutibu saratani na kufanyiwa upasuaji, zilimuathiri zaidi kiafya. Kutokana na madhara hayo, Serikali ilimchukua Chid Benz na kumpeleka katika kituo cha upataji nafuu cha Pili Missana Foundation kilichopo jijini Dar es Salaam na sasa amepona.


Ameongeza kuwa, kati watu hao milioni ambao kwa nyakati tofauti wamepatiwa matibabu bure na Serikali kote nchini wengi wao ni vijana.


"Tunamtoa Chid Benz kama mfano wa vijana ambao wamepatiwa tiba na Serikali na wanerudi katika hali yao ya kawaida, kwa wanaomzoea Chid Benz kabla ya kupata matibabu na kuchukuliwa na Serikali hali yake ilikuwa mbaya sana na walimzushia kifo."


Amesema, baada ya Serikali kumpatia matibabu sasa afya yake imeimarika na yupo tayari kuanza kuwahudumia wananchi kwa burudani kama zamani na kuhakikisha nchi inaendelea kufurahi kwa kuwa na mwanamuziki hodari.


Kwa upande wake, Chid Benz ameishukuru DCEA kwa kumuonesha moyo wa upendo, kwani awali alikata tamaa baada ya kuathiriwa na matumizi ya heroin na dawa tiba zenye asili ya kulevya, lakini sasa yupo imara.

"Kwa kawaida watu husema bahati haiji mara mbili, sasa hivi nipo sawa na karibuni nitarudi mtaani kuendelea na kazi zangu, ninaombeni ushirikiano wenu, ninaishukuru sana mamlaka, ninamshukuru Brother Lyimo (Kamishna Jenerali Lyimo) kwa kunisaidia, Dkt.Mapana nipo bega kwa bega nao na nitafanya kazi kwa bidii."

Aidha, Chid Benz ametoa angalizo kwa wasanii wenzake kuepuka matumizi ya dawa za kulevya kwani si tu kwamba zinaathiri afya, bali pia zinaua ndoto na kipaji.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Dkt.Kedmon Mapana ameishukuru DCEA kwa kazi kubwa iliyofanya kuhakikisha msanii Chid Benz anarejea katika hali yake.

Amesema, wakati baraza hilo likimkabidhi Chid Benz kwa mamlaka ili Serikali ikampatie matibabu hali yake ilikuwa mbaya zaidi, lakini leo ana afya njema na anatarajia kuanza kutekeleza majukumu yake ya kimuziki hivi karibuni.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Pili Missana Foundation, Bi.Pili Missana amewataka Watanzania kuondoa hofu kuhusu muonekano mpya wa Chid Benz.

Amesema, afya ya msanii huyo imeimarika na kuonekana mnene kutokana na matumizi sahihi ya lishe,na si makemikali ambayo alikuwa akiyatumia awali.

No comments:

Powered by Blogger.