MAONESHO YA 20 YA BIASHARA AFRIKA MASHARIKI KUVUTIA WENGI
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Gabriel Kenene.
Na Shagaka Suleiman, Mwanza
Zaidi ya watu 250,000 wanatarajiwa kutembelea maonesho ya biashara Afrika Mashariki yatakayofanyika katika uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza kwa siku 10 kuanzia 29 mwezi huu hadi Septemba 07 mwaka huu 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari Ijumaa Agosti 22, 2025 jijini Mwanza, Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Gabriel Kenene alisema washiriki katika maonesho hayo wamejiandaa vya kutosha kutoa huduma zao kwa wananchi watakaofika.
Alisema zaidi ya washiriki 500 wamealikwa kuleta huduma zao ambapo zaidi ya 100 watatokea nchi za nje huku kauli mbiu itakayopamba maonesho hayo ikisema "Biashara Kijani, Uchumi Mzunguko, Maisha Endelevu".
Kenene alisema lengo la maonesho hayo ni kufungua fursa kwa wafanyabiashara wa kada zote, wakulima, wenye viwanda,wajasiriamali, sekta binafsi, kutengeneza mtandao wa kibiashara katika nchi za Afrika Mashariki na Maziwa Makuu.
Vilevile aliongeza kusema kuwa maonesho hayo yanaitangaza Mwanza kuwa kitovu cha biashara Afrika Mashariki na Maziwa Makuu, kushindanisha makampuni, biashara mbalimbali na kutoa fursa kwa taasisi za umma kutoa elimu kwa umma kuhusu shughuli wanazofanya.
Kenene alisema bidhaa zitakazooneshwa na kuuzwa ni mashine na teknolojia, bidhaa za ujenzi, thamani za nyumbani na ofisini, bidhaa za kilimo na mifugo, bidhaa za usindikaji na vinywaji, bidhaa za huduma kama hoteli na utalii.
Aidha bidhaa za sanaa na kazi za mikono, bidhaa za uchapaji matangazo ya redio na televisheni, bidhaa za mawasiliano ya habari na huduma zinazotolewa na Taasisi za serikali, mashirika ya Umma na serikali za mitaa.
Aliongeza kusema bidhaa na huduma zingine zitakazofanyika ni uuzajins utengenezaji nguo za ngozi, mafunzo, huduma za ushauri, bidhaa za utalii, maliasili, kutangaza utalii wa Tanzania na vivutio vilivyopo Mkoa wa Mwanza na watakuwepo wanyamapori hai na michezo mbalimbali ya watoto itafanyika.
Kenene alisema mafanikio yanayotarajiwa ni kwa wafanyabiashara kuongeza mtandao wa biashara, kuongeza ubora wa bidhaa na kuboresha teknolojia, kupata masoko zaidi, makampuni ya kigeni kupata masoko, mawakala wa kuuza bidhaa zao na kubadilishana uzoefu.
Tazama BMG TV hapa chini
PIA>>> Bonyeza hapa kusoma zaidi
No comments: