LIVE STREAM ADS

Header Ads

TCRA yaendesha mafunzo kwa wanahabari na watangazaji Kanda ya Ziwa kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com


Na Kadama Malunde, Mwanza

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), imeendesha mafunzo kwa waandishi wa habari na watangazaji kutoka Kanda ya Ziwa, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuhakikisha taarifa zinazohusu Uchaguzi Mkuu wa 2025 zinaripotiwa kwa weledi, usahihi na kwa kuzingatia maadili ya taaluma ya habari.

Mafunzo hayo yamefanyika leo Agosti 7, 2025 katika ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania, jijini Mwanza na yamehusisha washiriki zaidi ya 120 kutoka mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Kigoma, Mara na Kagera.

Katika semina hiyo, washiriki wamewasilishiwa mada saba muhimu zinazolenga kuboresha uwezo wao wa kitaaluma, kukuza uelewa wa majukumu yao kuelekea uchaguzi, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya habari, vyombo vya dola na wadau wa uchaguzi kwa ujumla.
Mada ya kwanza imewasilishwa na Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ikieleza kwa kina namna wanahabari wanavyopaswa kuandika habari za uchaguzi kwa kuzingatia kanuni za kitaaluma, ukamilifu wa taarifa, usawa kwa vyama vya siasa, pamoja na kulinda amani na mshikamano wa kitaifa.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewasilisha mada kuhusu Kanuni za Utangazaji wa Uchaguzi kwa Vyama vya Siasa za mwaka 2020, ikifafanua masharti ya utoaji wa muda wa matangazo yanayohusu shughuli za uchaguzi, usimamizi wa maudhui ya kampeni na wajibu wa watoa huduma za utangazaji kuhakikisha usawa, uadilifu na uwazi katika kuripoti shughuli za uchaguzi.
Jeshi la Polisi kupitia mwakilishi wake Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini DCP David Misime, limewasilisha mada kuhusu wajibu wa wanahabari na vyombo vya dola katika kulinda usalama kipindi cha uchaguzi. Washiriki walifahamishwa kuhusu umuhimu wa ushirikiano baina ya pande hizo mbili katika kuripoti matukio ya kiusalama kwa njia salama, yenye kuzingatia taratibu za kisheria na za kiusalama.
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imewasilisha mada kuhusu maadili na sheria zinazowaongoza waandishi wa habari nchini, ikiangazia wajibu wa waandishi kuhakikisha taarifa zao hazivunji sheria, hazichochei chuki au vurugu na zinazingatia haki za watu wanaotajwa katika taarifa za habari.
Wataalamu wa maudhui ya utangazaji na habari kutoka Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC-UDSM), wamewasilisha mada kuhusu Mitandao ya Kijamii na Akili Bandia (AI) kuelekea Uchaguzi, iliyoeleza jinsi mitandao ya kijamii na teknolojia ya Akili Bandia (AI) inavyobadilisha mienendo ya uchaguzi, pamoja na changamoto za usambazaji wa taarifa potofu na athari zake kwa amani ya nchi. Waandishi walihimizwa kuwa makini na matumizi ya vyanzo vya kidijitali na kuhakikisha uthibitisho wa taarifa kabla ya kuchapisha.

TCRA imewasilisha pia mada kuhusu namna bora ya kuripoti migogoro na majanga wakati wa uchaguzi, kwa kuzingatia weledi, lugha inayotumika, na athari za taarifa hizo kwa umma. Washiriki walikumbushwa kuepuka kueneza hofu au taarifa zenye kuchochea hisia za uhasama.
Kwa upande wake Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ikiwakilishwa na Mkuu wa Mawasiliano Serikalini Innocent Mungy, imewasilisha mada kuhusu umuhimu wa kulinda taarifa za watu binafsi katika kipindi cha uchaguzi, hasa wakati wa ukusanyaji, uchakataji na usambazaji wa taarifa zinazomhusu mtu mmoja mmoja. Waandishi walihimizwa kufuata misingi ya faragha na ulinzi wa taarifa katika kazi zao za kila siku.

Mafunzo haya yamelenga kuongeza uelewa wa pamoja baina ya wanahabari, watangazaji, vyombo vya dola na taasisi za uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, haki na ufanisi. Aidha, yamebainisha umuhimu wa teknolojia na matumizi yake sahihi katika kuripoti uchaguzi katika enzi ya kidijitali.


No comments:

Powered by Blogger.