LIVE STREAM ADS

Header Ads

Walinzi wanyamapori wapewa 'tano" kuongezeka wanyama Burunge WMA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

  

Mwandishi wetu,Babati

Mamlaka ya Usimamizi wanyamapori nchini(TAWA) kwa kushirikiana na Taasisi ya uhifadhi ya Chem Chem na halmashauri ya wilaya ya Babati, wameadhimisha siku ya walinzi wa wanyamapori Duniani,  huku wakitaja mafanikio kadhaa ikiwepo kuongeza idadi ya wanyamapori   eneo la hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori ya Burunge..

Kila mwaka, Julai 31, Shirikisho la kimataifa la walinzi wa wanyamapori(IRF) huadhimisha siku ya walinzi wa wanyamapori ili kuenzi kazi nzuri inayofanyika, lakini pia kuwakumbuka  walinzi waliopata changamoto kazini na Kauli mbiu ya mwaka huu ni Walinzi Wanaoendeleza Uhifadhi wa Mabadiliko.

Wakizungumza  katika Maadhimisho hayo, yaliyoambata na mazoezi ya vitendo ya Askari wa ulinzi wa Chem Chem, TAWA na Askari wa Wanyamapori wa halmashauri ya Babati ,katika  eneo la Burunge WMA, katika moja ya kambi za ulinzi za Chem Chem, viongozi wa Askari hao,walieleza ushirikiano baina yao umeleta mafanikio makubwa katika uhifadhi.

Askari wa Uhifadhi wa TAWA Daraja la pili, James Misuka alisema Walinzi wa Wanyamapori na Uhifadhi wa mazingira, wamekuwa na mchango mkubwa katika  kuimarisha Uchumi wan chi, kwani sasa wanyamapori hasa Tembo wameongezeka  na kuvutia watalii.

“Jamii imekuwa ikinufaika moja kwa moja na uhifadhi kutokana na fedha za Utalii, kutumika kujenga shule, Barabara, kuboresha huduma za afya, maji na nyingine nyingi hii leo tunapoadhimisha siku yetu tunaona mafanikio”alisema

Msimamizi wa miradi ya Maendeleo ya jamii ya Chem Chem , ambao wamewekeza shughuli za Uhifadhi na Utalii wa picha katika eneo la Burunge WMA,  Napendaeli  Wazoeli alisema Chem Chem inathamini sana mchango wa Walinzi katika uhifadhi ambao sasa umeweka usawa wa kijinsia pia.

“Timu yetu ya walinzi imezingatia usawa wa kijinsia  na maendeleo ya kiteknolojia  katikati ya ulinzi na uhifadhi na sasa tuna walinzi mahiri wa kike, wakiwepo Brenda na Nasra na hivyo tumeweza kuimarisha ulinzi lakini pia na ushirikiano na jamii”alisema

Alisema Walinzi  wa uhifadhi wamefanikiwa  kupunguza sana migongano baina ya wanyamapori hasa Tembo na binaadamu  kwani wamekuwa na ushirikiano mzuri, askari wa Chem Chem,Askari wa TAWA, Burunge WMA na halmashauri ya Babati.

Mkuu wa Walinzi wa Chem chem,Hamis Chamkuru alisema,wamepata faraja uongozi wa Chem Chem kuandaa maadhimishi hayo kwani inaonekana unatambua kazi kubwa  wanayofanya katika ulinzi wa wanyamapori na mazingira.

“Tangu mwaka 2017 tumekuwa na ushirikiano wa Pamoja wa walinzi katika eneo hili, tumeweza kutoa elimu ya uhifadhi katika jamii na hivyo kupunguza sana matukio ya ujangili na uharibifu wa mazingira katika eneo la Burunge WMA na mapito ya Wanyama ya Kwakuchinja”alisema

Alisema wamefanikiwa kuwatia mbaroni, majangili kadhaa ndani ya eneo la Burunge WMA na nje ya eneo hilo  na mtandao wao umeweza kudhibitiwa na wengi wamefungwa.

Afisa Wanyamapori katika Halmashauri ya Babati,  Godluck Kalambane alisema wanathamini sana siku ya walinzi wa wanyamapori kwani inaonesha kazi nzuri ambayo wanafanya lakini pia kukumbuka ambao wamepata madhira kadhaa kazini.

“Tumekuwa na ushirikiano mkubwa sisi kama walinzi lakini pia na wananchi ambao wanazunguka maeneo ya hifadhi”alisema

Askari wa ulinzi wa kike, Brenda Julius aliwataka wanawake kutoogopa kazi za ulinzi wa wanyamapori kwani  ni nyepesi lakini inahitaji ujasiri.

“Wanawake wasiogope kazi hii, haina shida licha ya kuifanya usiku na mchana hii ni kazi ya ulinzi wa rasilimali za nchi yetu na natoa wito wanawake zaidi wajitokeze”alisema.

Siku ya ulinzi wa wanyamapori ilianzishwa Julai 31 mwaka 1992 nchini Uingereza   na ilifatiwa na kuundwa shirikisho la Kimataifa la  walinzi wa Wanyamapori(IRF) mwkama  2007 Julai 31 na ndio ilianza rasmi kuadhimishwa siku hii.

No comments:

Powered by Blogger.