Wananchi Kyerwa Wameaswa kuwasomesha Watoto ili Kutumia Fursa za Michezo
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

Kyerwa, Kagera – Wazazi na walezi wilayani Kyerwa wametakiwa kuhakikisha wanawasomesha watoto wao kwa nguvu zote ili waweze kutumia kikamilifu fursa zote za maendeleo, zikiwemo zile za michezo ambazo zinaweza kuwa msingi wa maisha yao ya baadaye. Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Abdulmajid Nsekela (Abdulmajid Nsekela Foundation), Abdulmajid Mussa Nsekela wakati wa uzinduzi wa Uwanja wa Nsekela uliofanyika wilayani humo, jana.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi huo, Nsekela alisema kuwa, ujenzi wa uwanja huo umekuwa na lengo la kuwapa vijana wa wilaya ya Kyerwa chombo cha kujikuza na kuibua na talanta katika michezo.

"Uwanja huu ni fursa kwa vijana wa Kyerwa, na siku moja timu kubwa za Tanzania zitakuja kucheza hapa," alisema Nsekela kwa shauku.
Aliongeza kuwa, "Hata hivyo, naomba kuwaasa wazazi kuwa michezo ni nyongeza kwa elimu na si badala yake, hivyo ni vyema kwa wazazi kuwasaidia mtoto wako kuwa bora darasani, ndipo talanta yake kiwanjani itakapokuwa na msingi imara."

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Fatma Mwassa, aliyekuwa mgeni rasmi, alimtaja Nsekela kwa kukumbuka asili yake na kuwekeza kwenye mradi mkubwa na wenye tija kwa wananchi wa Kyerwa.
"Ninamshukuru sana Ndugu Nsekela kwa kuwekeza kwenye maeneo haya. Hii ni kumbukumbu ya kudumu na itaweza kuchangia katika kuleta maendeleo nyumbani kwao," alisema Mwassa.
Aidha, alionya wasimamizi na jamii kwa ujumla kuutunza uwanja huo kwa dhati na kuuhifadhi kwa manufaa ya vizazi vijavyo, akikataza vitendo vya uharibifu.
Kwa upande wake Msemaji wa Taasisi ya Abdulmajid Nsekela (Abdulmajid Nsekela Foundation), Tully Esther Mwambapa, alisema kuwa uwanja huo sio wa mpira wa miguu pekee, bali utajumuisha viwanja kamili vya mpira wa kikapu na pete, pamoja na eneo maalum la michezo ya riadha.
Aliongeza kuwa uwanja huo umewekwa majukwaa ya kisasa na salama kwa ajili ya watazamaji, na utakuwa ni wa kiwango cha kimataa.
Wadau wa michezo na viongozi wa jamii wamepongeza juhudi hizo za kuwezesha kupata uwanja mpya, kwani utawavutia vijana kuonyesha na kulea talanta zao kitaalamu. Zaidi ya hayo, wamebainisha kuwa uwanja huo utajenga uchumi wa ndani kwa kuwapa fursa wadau mbalimbal wakiwemo wakulima wadogo, wafanyibishara wa vyakula na vinywaji, na wauzaji wa vifaa vya michezo kuingia kwenye mnyororo wa uchumi unaozaliwa na shughuli za kimichezo.
Hatua hiyo ya uwekezaji inaonekana kuwa chanzo kipya cha furaha, umoja na matumaini kwa wananchi wa Kyerwa na mkoa mzima ya Kagera.



No comments: