TAMASHA KUBWA LA MICHEZO "SIKU YA WANA' STAND UNITED KUFANYIKA OKTOBA 4,2025
Mwenyekiti wa Tamasha la Siku ya Wana 'Yes! Yes! Yes! Chrispin Kakwaya, akielezea kuhusu maandalizi ya tamasha hilo. Picha na Kadama Malunde
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 25, 2025, Mwenyekiti wa Tamasha hilo, Chrispin Kakwaya, amesema maandalizi yanaendelea vizuri na mashabiki wa Stand United watapata siku ya kipekee kuanzia asubuhi hadi jioni.
“Kutakuwa na michezo ya mbio za baiskeli kwa wanaume na wanawake, burudani kutoka kwa wasanii wa Kanda ya Ziwa na Shinyanga, pamoja na michezo ya utangulizi ikiwemo mpambano kati ya timu za Bajaji na Bodaboda, Soko Kuu na Soko la Majengo, kisha Dabi ya Upongoji FC na Ibinzamata,” amesema Kakwaya.
Ameongeza kuwa baada ya michezo hiyo, kutafanyika utambulisho wa wachezaji wapya wa Stand United, hatua itakayofuatiwa na mchezo wa kirafiki kati ya Stand United na timu kutoka Ligi Kuu, ambayo itatajwa siku chache kabla ya tamasha.
“Natoa wito kwa wananchi na wapenzi wa Stand United, mashirika na taasisi mbalimbali kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu yao. Viingilio vitakuwa ni Sh. 5,000 kwa mzunguko, Sh. 10,000 kwa VIP, na VVIP watakuwa na kadi maalum,” ameongeza Kakwaya.
Aidha, amesema tamasha hilo litatanguliwa na jogging ya pamoja itakayoshirikisha wanamichezo na Mashabiki wa Stand United.
Kwa upande wake, Msemaji wa Stand United, Ramadhan Zorro, amesema tamasha hilo litakuwa la aina yake, tofauti na matamasha mengine yaliyowahi kuandaliwa na timu nyingine.
“Tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kuona kikosi kipya tulichosajili na pia tunakaribisha wadhamini kushirikiana nasi kuhakikisha Stand United inarejea kwenye hadhi yake kubwa,” amesema Zorro.
No comments: