HABARI SAHIHI NI SILAHA YA DEMOKRASIA – SALMA ABDUL AWAASA WAANDISHI WA HABARI
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

Na Mwandishi wetu - Tabora



Mjumbe wa Bodi ya UTPC, Salma Abdul akifunga mafunzo maalum ya siku mbili kwa waandishi wa habari mkoani Tabora yaliyojikita katika kukabiliana na changamoto za habari potofu (fake news)

Mjumbe wa Bodi ya UTPC, Salma Abdul akifunga mafunzo maalum ya siku mbili kwa waandishi wa habari mkoani Tabora yaliyojikita katika kukabiliana na changamoto za habari potofu (fake news).
Picha ya pamoja washiriki wa mafunzo
Na Mwandishi wetu - Tabora
Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), umekamilisha mafunzo maalum ya siku mbili kwa waandishi wa habari mkoani Tabora yaliyojikita katika kukabiliana na changamoto za habari potofu (fake news), misinformation na disinformation, hususani kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akifunga rasmi mafunzo hayo leo Oktoba 2, 2025, Mjumbe wa Bodi ya UTPC, Salma Abdul, amewataka waandishi wa habari waliopata mafunzo hayo kutumia ujuzi na mbinu walizojifunza kusaidia jamii kupambana na taarifa potofu ambazo zimekuwa tishio kubwa duniani.
“Mafunzo haya si kwa ajili yenu peke yenu. Ni wajibu wenu kuyatumia kulinda jamii dhidi ya upotoshaji wa taarifa. Wakati huu wa uchaguzi, waandishi wa habari mnahitajika zaidi kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, zenye kuaminika na zinazojenga, si kubomoa,” amesema Salma Abdul.
Andrew Marawiti
Kwa upande wake, Afisa Programu wa UTPC, Andrew Marawiti, amebainisha kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Ukweli Kwanza wenye lengo kuu la kuongeza weledi wa waandishi wa habari na uimara wa wananchi dhidi ya upotoshaji wa taarifa.
“Tunataka angalau waandishi 100 wapate ujuzi wa mbinu za kupambana na misinformation, disinformation, fact-checking na matumizi ya teknolojia ikiwemo Artificial Intelligence (AI) katika kuthibitisha ukweli wa habari. Pia tunalenga kuwawezesha waandishi chipukizi, hususani wanawake, kuwa mstari wa mbele katika mapambano haya,” amesema Marawiti.
Mwezeshaji wa mafunzo Kadama Malunde
Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Kadama Malunde, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Malunde 1 Blog, ameeleza mbinu za kutambua na kupambana na taarifa potofu, akibainisha kuwa mitandao ya kijamii imekuwa chanzo kikubwa cha upotoshaji hasa nyakati za uchaguzi, majanga au masuala ya afya.
Aidha, Afisa kutoka JamiiAfrica, Innocent Mangu, amepongeza hatua ya UTPC kuwekeza katika kujenga uwezo wa waandishi wa habari.
Innocent Mangu
“JamiiAfrica tunaamini kuwa bila taarifa sahihi, wananchi hawawezi kufanya maamuzi bora hasa kipindi cha uchaguzi. Ndiyo maana tunashirikiana na UTPC kuhakikisha waandishi wa habari wanapata mbinu bora za kuhakiki taarifa na kupambana na propaganda. Tunawategemea ninyi waandishi kuendelea kuwa ngao ya jamii dhidi ya upotoshaji,” amesema Mangu.
Washiriki wamepatiwa mbinu mbalimbali za uthibitishaji wa habari ikiwemo matumizi ya Akili Unde, kugundua asili ya picha na video, kulinganisha taarifa na vyanzo vinavyoaminika, na kusoma zaidi ya vichwa vya habari ili kuepuka kupotoshwa.
Mafunzo haya yamefadhiliwa na Ubalozi wa Uholanzi kupitia ushirikiano wa UTPC na JamiiAfrica,na yanalenga kuhakikisha waandishi wa habari wanabaki kuwa nguzo muhimu ya ukweli na weledi, ili kuongeza imani ya wananchi kwa vyombo vya habari na kuimarisha mchakato wa uchaguzi mkuu ujao.



No comments: