RIDHIWANI KIKWETE AWASHUKURU WANANCHI WA MBEYA KUSHIRIKI KILELE CHA MWENGE WA UHURU 2025

Katika salamu zake, Waziri Kikwete amesema kuwa mwaka huu Mwenge wa Uhuru umeandika historia mpya na ya kipekee, sio tu kwa urefu wa mbio na idadi ya miradi iliyotembelewa, bali pia kwa ubora wa maandalizi, ushiriki wa wananchi, na kwa mara ya kwanza, ushiriki wa watoto wenye ulemavu wa viungo katika halaiki ya taifa. Amesema “Hii ni historia ambayo hatuwezi kuisahau. Ushiriki wa watoto wenye ulemavu kwenye halaiki ni ishara kuwa Mwenge wa Uhuru unawakilisha Watanzania wote, bila ubaguzi,”.
Shughuli za kilele hicho zilianza na Misa Takatifu ya kumuombea Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, iliyoongozwa na Kanisa Katoliki. Baadaye, wananchi walijumuika kwenye hafla ya kufunga Maonyesho ya Kazi za Vijana yaliyodumu kwa siku saba katika viwanja vya Uhindini, ambapo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, alikuwa Mgeni Rasmi.
Ameongeza kuwa maonyesho hayo yalionesha wazi vipaji, ubunifu na juhudi za vijana katika sekta mbalimbali na kwamba ushiriki mkubwa ulioshuhudiwa ni kiashiria kuwa vijana wako tayari kuchangia maendeleo ya taifa.“Maonyesho haya yamekuwa na mafanikio makubwa. Vijana wameonyesha uwezo mkubwa wa ubunifu, na hii ni dalili njema kwa mustakabali wa taifa letu,”
Aidha, Kikwete ametangaza kuwa Mwenge wa Uhuru 2026 utafika kilele chake katika Mkoa wa Rukwa, baada ya kuwashwa katika Mkoa wa Kusini Pemba na kupitia mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar. Katika kilele hicho, kutafanyika pia Kongamano la Kitaifa la Vijana pamoja na Maonyesho ya Kazi za Vijana Kitaifa.
Akihitimisha salamu zake, amewapongeza wananchi wa Mbeya kwa hamasa na mshikamano waliouonesha katika wiki nzima ya shughuli za Mwenge. “Wanambeya mmekuwa mfano wa kuigwa. Ushiriki wenu katika misa, kongamano la vijana na maonyesho umetufariji sana. Mmeuenzi Mwenge wa Uhuru na mmeonyesha kuwa kweli ni tunu ya umoja na maendeleo ya taifa letu,” alisema.
#Miaka60YaMwengeWaUhuru
#MwengeWaMaendeleo
#MwengeNaVijana
#VijanaNiNguvuYaTaifa
#TunamuenziBabaWaTaifa
No comments: