LIVE STREAM ADS

Header Ads

WAUMINI ILALA WAMUOMBEA SAMIA USHINDI

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wakazi wa Ilala jijini Dar es Salaam wamefanya dua maalum yenye lengo la kuliombea Taifa amani na kumwombea mgombea urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amalize kampeni zake kwa salama na apate ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Dua hiyo iliyofanyika Jumamosi Oktoba 10 nyumbani kwa Issa Kivina, anayefahamika zaidi kama Mr Cap, ilihudhuriwa na mamia ya wananchi, viongozi wa dini na wanasiasa wa chama hicho.

Tukio hilo lilihusisha sala kumsifu Mungu, na hotuba fupi zilizogusa mioyo ya wengi kuhusu umuhimu wa kudumisha amani wakati wa kampeni na uchaguzi.

Mgeni rasmi, Mussa Azan Zungu, mgombea ubunge wa Jimbo la Ilala, alitumia nafasi hiyo kuhimiza wananchi kupuuza kauli zinazoweza kuleta mgawanyiko au kuchochea vurugu.

“Watanzania tumepewa zawadi kubwa ya amani. Rais Dkt. Samia ameshaeleza kuwa hali ya nchi ni shwari, na vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kulinda utulivu huo. Hivyo ni wajibu wetu kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kumpa kura za ushindi yeye na wagombea wa CCM” alisema Zungu.

Zungu aliongeza kuwa kampeni zenye heshima na kuzingatia hoja ndizo zitakazojenga Taifa lenye umoja na siasa safi, akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda amani iliyojengwa kwa miaka mingi.

Kwa upande wake, Mr Cap, mratibu wa dua hiyo, amesema lengo lake lilikuwa ni kumshukuru Mungu kwa kiongozi aliyejaa hekima kama Rais Samia, na kumuombea ulinzi dhidi ya majaribu, husuda na balaa lolote linaloweza kujitokeza katika kipindi hiki cha uchaguzi.

“Dua hii ni ya kumkabidhi Mama Samia mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Tumeomba apate mafanikio mema na aendelee kuwa kiongozi wa neema kwa Watanzania wote. Amani ya nchi hii ni tunu, na dua zetu ni sehemu ya kuitunza” alisema Mr. Cap.

Katika kuonesha upendo wake wa dhati kwa Rais Samia, Mr Cap alichinja ngamia kama sadaka maalum, akisema ni ishara ya upendo, utiifu na imani yake kuwa kiongozi huyo ataendelea kuongoza kwa busara.

“Ngamia huyu ni sadaka yangu binafsi kama shukrani na dua ya amani. Ni alama ya upendo wangu kwa Mama Samia na taifa letu” aliongeza Mr. Cap huku waumini wakimshangilia.

Baadhi ya washiriki wa dua hiyo wameisifu hatua hiyo wakisema imeleta faraja na kuonesha namna wananchi wanavyoweza kutumia maombi kama njia ya kuimarisha mshikamano wa kitaifa.

“Hii ni dua ya kipekee. Imetukumbusha kuwa siasa ni za kupita, lakini amani ni ya kudumu,” alisema Ali Bakari, mmoja wa waliohudhuria.

Naye Mwanahawa Juma, mkazi wa Ilala Boma, alihamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura.

“Mama Samia anaungwa mkono na wanawake wengi, lakini tunapaswa kujitokeza kwa wingi kumpa kura nyingi zaidi. Ni wajibu wetu kama wamama kuhakikisha tunaweka alama tatu za ushindi” alisema.

Hafla hiyo ilimalizika kwa waumini kushikana mikono na kusoma dua ya pamoja ya kuliombea Taifa utulivu, uchumi imara na uchaguzi wenye amani.

“Tumeomba Tanzania ibaki kuwa kisiwa cha amani, na viongozi wote wapewe busara za kuongoza kwa haki” alisema mmoja wa viongozi wa dua hiyo kabla ya shughuli kufungwa rasmi.
#KaziInaongea

No comments:

Powered by Blogger.