LIVE STREAM ADS

Header Ads

TANZANIA NA QATAR ZASAINI HATI YA MAKUBALIANO KUTAMBUA VYETI VYA MABAHARIA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Malick Salum na Mhandisi Abdulaziz Abdullah Al-Sulait, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi wa Qatar, akisaini kwa niaba ya nchi yake wakisaini Hati ya kutambuliana vyeti vya Mabaharia na Qatar katika hafla iliyofanyika London.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Malick Salum na Mhandisi Abdulaziz Abdullah Al-Sulait, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi wa Qatar wakiwa wameshikana mkono mara baada kusaini Hati ya Makubaliano ya kutambuliana vyeti vya Mabaharia na Qatar katika hafla iliyofanyika London.
***


Serikali ya Tanzania na Serikali ya Qatar leo, tarehe 24 Novemba 2025, zimesaini hati ya makubaliano (MoU) ya kutambuliana vyeti vya mabaharia katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika jijini London. Hafla hiyo imefanyika pembezoni mwa mkutano wa 34 wa Baraza Kuu la Shirika la Bahari Duniani na kuhudhuriwa na viongozi pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya bahari.

Kwa upande wa Tanzania, makubaliano hayo yamesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Malick Salum, huku Mhandisi Abdulaziz Abdullah Al-Sulait, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi wa Qatar, akisaini kwa niaba ya nchi yake.

Kupitia MoU hii, pande zote mbili zinatarajia kuboresha viwango vya umahiri, usalama na ubora katika taaluma ya ubaharia, sambamba na kuendeleza mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Qatar.

Hatua hii inatarajiwa kuongeza ajira kwa mabaharia wa Kitanzania katika meli zilizosajiliwa au kuendeshwa na kampuni za Qatar, kwani hawatalazimika kupitia upya taratibu za uthibitishaji wa vyeti pamoja na kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usafirishaji baharini kati ya nchi hizo mbili.

Aidha makubaliano haya yatawezesha mabaharia kupata maslahi bora na fursa zaidi za kazi kwenye masoko yenye ushindani wa juu na kunachochea uhamishaji wa ujuzi na utaalamu wa kimataifa, kwa kuwa mabaharia watafanya kazi katika majukwaa yenye viwango vya juu vya teknolojia na usalama pamoja na kuimarisha uwezo wa Tanzania katika utoaji wa mafunzo ya ubaharia, kwani vyuo na vyeti vyake vitakuwa na uhalali mpana zaidi kimataifa.

No comments:

Powered by Blogger.