RC SENDIGA AANZA ZIARA YA KATA KWA KATA HANANG’, AKAGUA MIRADI NA KUTATUA KERO ZA WANANCHI
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Na Ruth Kyelula, Manyara
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, ameanza ziara maalumu ya ukaguzi wa miradi na kusikiliza kero za wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’, ikiwa ni sehemu ya msisitizo wake wa kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kauli mbiu “Tunavua buti ama hatuvui, tukutane site.”
Ziara hiyo iliyoanza Desemba 4, 2025, inafanyika Kata kwa Kata na imehusisha viongozi wote wa taasisi za umma na binafsi kutoka katika mkoa huo.
Katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tatu, RC Sendiga amekagua miradi mbalimbali ikiwemo jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ pamoja na ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Waret. Aidha, ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa shule ya awali na msingi Semonyan iliyopo Kata ya Mogitu.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa amekabidhi nyumba kwa mmoja wa waathirika wa maporomoko ya tope yaliyotokea Desemba 3, 2023, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kuendelea kuwasaidia wananchi waliopoteza makazi.
Akiwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Waret na kijiji cha Gehandu, RC Sendiga alifanya mikutano ya hadhara na kusikiliza kero za wananchi moja kwa moja, ambapo masuala kadhaa ya maendeleo na changamoto za huduma za kijamii yalijadiliwa na kupatiwa ufumbuzi.

Alikagua pia madarasa mawili ya shule ya msingi Gisamjanga pamoja na mradi wa ujenzi wa bweni la wavulana katika shule ya sekondari ya Mwahu.
Akizungumza wakati wa ukaguzi, RC Sendiga aliwataka wananchi kuunga mkono juhudi za serikali kwa kupanda miti ya matunda na ya kivuli katika maeneo ya miradi, hususan katika shule mpya pamoja na miradi mingine ya kijamii.
“Ni muhimu kuhakikisha miradi ya ujenzi wa shule inakamilika kwa wakati ili watoto wetu waanze masomo mwezi Januari bila vikwazo,” alisema.
Ziara hiyo inaendelea katika maeneo mengine ndani ya Wilaya ya Hanang’, ikiwa na lengo la kusimamia utekelezaji wa miradi, kuwahamasisha wananchi kushiriki katika maendeleo na kuimarisha utatuzi wa changamoto kwa wakati.



















No comments: