NIMR: TAFITI ZIBADILISHWE KUWA HATUA ZA VITENDO
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
๐8 Januari, 2026,
♻️ Dar es Salaam
Mdahalo wa sera ulioandaliwa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) umeibua mapendekezo mbalimbali yanayolenga kuimarisha matumizi ya matokeo ya tafiti katika maandalizi, kinga na mwitikio dhidi ya magonjwa ya mlipuko yanayoibuka na kujirudia nchini.
Mdahalo huo umehusisha wadau mbalimbali ikiwepo watafiti, na watunga sera kutoka sekta mbalimbali ikiwepo Wizara ya afya, Wizara ya Elimu, TAMISEMI.
Pia umehusisha taasisi mbalimbali za utafiti ikiwepo Taasisi ya Utafiti Zanzibar (ZAHRI), Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) pamoja na wengine. Lengo hasa la mjadala huu ni kuhusu umuhimu wa kutafsiri matokeo ya utafiti kuwa hatua za utekelezaji ndani ya sera na mipango ya kitaifa katika kupambana na magonjwa ya mlipuko
Mdahalo huo umefunguliwa rasmi na Dkt. Ahmad Mohamed Makuwani, Mkurugenzi wa Huduma ya Afya ya Uzazi, Magonjwa ya Wanawake na Watoto kutoka Wizara ya Afya, akimwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali. Dkt. Makuwani alisisitiza kuwa matumizi ya matokeo ya tafiti ni nguzo muhimu katika kujenga mfumo imara wa afya unaoweza kukabiliana kwa ufanisi na milipuko ya magonjwa, aliwahimiza washiriki kuhakikisha matokeo ya tafiti yanabadilishwa kuwa sera na vitendo vinavyoweza kuchochea majibu ya haraka na bora pindi mlipuko utapotokea, hali ambayo inaendelea kuweka shinikizo kwa huduma za afya nchini.
Katika mdahalo huo, jukumu la NIMR katika kuzalisha na kuratibu tafiti zinazolenga kusaidia sera lilisisitizwa, sambamba na umuhimu wa kuimarisha uhusiano kati ya matokeo ya tafiti za kisayansi na maamuzi ya kisera yanayofanywa ndani ya sekta ya afya. Washiriki pia walibainisha umuhimu wa kuimarisha tafiti za ndani, hususani utafiti wa tiba asili, wakitaja uzoefu wa mlipuko ya UVIKO 19 kama mfano wa jinsi tafiti za tiba asili zilivyosaidia jamii wakati wa mlipuko.
Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Profesa Said Aboud, amewashukuru washiriki kwa michango yao na kueleza kwamba tafiti zinazofanywa na taasisi hiyo zinalenga kuboresha mfumo wa afya na kugusa maisha ya wananchi wa kawaida; kwa hivyo, ni muhimu kuimarisha ushirikiano wa karibu kati ya NIMR na wadau mbalimbali ili matokeo ya mdahalo huu yaweze kuingizwa katika sera na mipango ya taifa.
Profesa Aboud alisema mdahalo umewezesha taasisi na wadau kubaini mapungufu na kuweka mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha maandalizi, kinga na majibu dhidi ya milipuko ya magonjwa.
Washiriki wa mdahalo walitoa mapendekezo kadhaa ikiwa ni pamoja na:
๐Kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tahadhari za mapema kwa magonjwa ya mlipuko.
๐Kuweka uwekezaji zaidi katika tafiti za afya ya umma.
๐ Kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za utafiti, serikali na wadau wa maendeleo.
๐Kuziba mapengo ya taarifa katika ngazi za chini za utoaji huduma za afya.
๐ Kuongeza matumizi ya takwimu na matokeo ya tafiti katika maamuzi ya kisera.
๐ Kuimarisha mawasiliano ya hatari kwa jamii na kuhakikisha mipango ya maandalizi inazingatia usawa na mahitaji halisi ya jamii.
Akihitimisha mdahalo huo, Profesa Aboud ameahidi kwamba NIMR itaendelea kudumisha ushirikiano na wadau mbalimbali na kuhakikisha mapendekezo yote yaliyotolewa katika mdahalo huu yanaingizwa katika sera na mipango ya taifa kwa lengo la kuboresha afya na ustawi wa wananchi.
“Tunathamini sana uwepo na michango ya wadau wote katika mdahalo huu. Matokeo ya mdahalo huu yataendelea kutumika katika sera na programu za taifa ili kuboresha afya na ustawi wa wananchi,” amesema Profesa Aboud.
#MatokeoYaTafiti
#MagonjwaYaMlipuko
#UtafitiWaAfya
#SeraYaAfya
#MatumiziYaTafiti
#AfyaYaUmma













No comments: