TISEZA YAHAMASISHA MIUNDOMBINU BORA KAMA KICHOCHEO KIKUU CHA KUVUTIA NA KULINDA UWEKEZAJI
Viongozi kutoka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) wakitembelea shule ya msingi Savannah iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga
Meneja wa Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani kutoka TISEZA, Felix John akizungumza baada ya kutembelea uwekezaji katika sekta ya elimu Shule ya Msingi na Sekondari Savannah Manispaa ya Shinyanga.
Na Mwandishi wetu _ Malunde 1 blog
Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imeendelea kuimarisha mkakati wa kuhamasisha uwekezaji wa ndani kwa kufanya ziara ya kikazi mkoani Shinyanga, ikisisitiza umuhimu wa miundombinu bora kama kichocheo kikuu cha kuvutia na kulinda uwekezaji.
Akizungumza leo Januari 29 2026 baada ya ukaguzi wa mradi wa uwekezaji katika sekta ya elimu uliofanyika katika Shule ya Msingi na Sekondari Savanah, Meneja wa Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani kutoka TISEZA, Felix John, amesema serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara ili kupunguza gharama na hatari kwa wawekezaji.
“Serikali inaweka mazingira rafiki kwa mwekezaji kwa kuimarisha miundombinu muhimu kama maji, umeme, barabara na mawasiliano katika maeneo yote yaliyotengwa kwa uwekezaji,” amesema John.
Ameeleza kuwa uwepo wa miundombinu hiyo huongeza tija ya miradi, kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ushindani wa Tanzania kama kitovu cha uwekezaji wa kikanda.
Uwekezaji wa Elimu Watajwa Kuwa Mfano wa Thamani ya Ndani
Katika ziara hiyo, TISEZA imekagua uwekezaji mkubwa wa sekta binafsi katika Shule ya Savannah, unaotajwa kuwa mfano wa uwekezaji wa kijamii wenye mchango wa moja kwa moja kiuchumi na kijamii katika mkoa huo.
Mkuu wa shule hiyo, Wema Kanyika, amesema taasisi hiyo inahudumia jumla ya wanafunzi 936 kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita.
“Tuna wanafunzi 512 wa elimu ya awali na msingi, pamoja na wanafunzi 424 wa sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita. Shule ina wafanyakazi 50 wanaoishi ndani ya eneo la shule,” amesema Kanyika.
Ameongeza kuwa uwekezaji huo unafanyika katika eneo la hekta 80, likiwa na miundombinu jumuishi ikiwemo Ufugaji wa ng’ombe kwa ajili ya uzalishaji wa maziwa na nyama kwa matumizi ya shule, Visima vya maji kwa uhakika wa upatikanaji wa maji na Bustani za miti ya matunda kwa lishe na mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi.
Muundo huo unaonyesha mwelekeo wa uwekezaji unaojitegemea kwa sehemu katika mahitaji ya chakula na huduma muhimu, hali inayopunguza gharama za uendeshaji kwa muda mrefu.
Shinyanga Yajipanga Kuwa Kitovu cha Uwekezaji
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amesema mkoa huo umejipanga kimkakati kupokea uwekezaji mkubwa zaidi kupitia maeneo maalum yaliyotengwa rasmi.
“Katika mkoa wa Shinyanga kuna maeneo mawili makubwa ya uwekezaji ambayo ni Buzwagi na Nyanshimbi. Maeneo haya yanaendelea kuboreshwa miundombinu ili kuhakikisha hakuna kikwazo kwa mwekezaji,” amesema Mhita.
Ameongeza kuwa uwepo wa bandari kavu (dry port) mkoani humo unatarajiwa kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo, kupunguza gharama za usafirishaji na kuifanya Shinyanga kuwa lango muhimu la biashara kwa ukanda wa Ziwa na nchi jirani.
Mtazamo wa Kiuchumi
Hatua za TISEZA kuunganisha uhamasishaji wa uwekezaji na uboreshaji wa miundombinu zinaonekana kulenga: Kuvutia wawekezaji wa ndani kabla ya kutegemea zaidi mitaji ya nje, Kukuza ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja na Kuchochea maendeleo ya mnyororo wa thamani katika sekta kama elimu, kilimo, ujenzi na huduma.
Shinyanga inaibuka kama moja ya mikoa inayolengwa kimkakati katika ramani ya uwekezaji wa ndani, huku miundombinu, ardhi iliyotengwa na miradi ya kimkakati kama bandari kavu vikionekana kuwa vivutio vikuu kwa wawekezaji wapya.
Mkuu wa shule ya Savannah Wema Kanyika akieleza uwekezaji katika sekta ya elimu







No comments: