TISEZA YATOA VIVUTIO KWA UPANUZI WA MRADI WA HOSPITALI MWANZA
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com


Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imetembelea mradi wa Hospitali ya Kamanga Medics (Kamanga Medics Hospital) iliyopo eneo la Nyegezi jijini Mwanza, ambao kwa sasa uko katika hatua ya upanuzi.
Hospitali hiyo inamilikiwa na wawekezaji Watanzania, ikiongozwa na Dkt. Rodrick Kabangila ambaye ni Mmiliki na Mkurugenzi Mtendaji wa mradi huo.
Mradi wa upanuzi wa Hospitali ya Kamanga Medics umesajiliwa rasmi na TISEZA na unastahili kunufaika na vivutio mbalimbali vya uwekezaji vinavyotolewa na Serikali, ikiwemo vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi.
Miongoni mwa vivutio hivyo ni pamoja na msamaha wa ushuru wa forodha wakati wa uingizaji wa mitambo, mashine pamoja na bidhaa za mtaji zinazohitajika katika uendeshaji wa hospitali, kama vile vitanda vya hospitali, mashuka na vifaa vingine muhimu vya tiba.
Kwa mujibu wa mpango wa uwekezaji, thamani ya mtaji wa mradi huo inakadiriwa kuwa kati ya shilingi bilioni 27 hadi bilioni 30 za Kitanzania.
Hospitali hiyo inatarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja kwa wafanyakazi kati ya 350 hadi 380 wa kudumu.
Hospitali ya Kamanga Medics imejengwa katika eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 1,800 na ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa hadi 1,000 kwa ujumla.
Kwa sasa hospitali ina vitanda 200, ikihudumia wagonjwa wa nje takribani 600 kwa siku, huku wagonjwa wa kulazwa wakiwa wastani wa 80.
Hospitali hiyo ni ya binafsi na imetambuliwa kama hospitali ya rufaa ya kanda (Zonal Referral Hospital), ikitoa huduma za kibingwa na kibobezi kwa wakazi wa Mkoa wa Mwanza na mikoa ya jirani.
Mradi huu ulianzishwa mwaka 2013 na umeendelea kupanuliwa kwa lengo la kuongeza uwezo wa utoaji wa huduma bora za afya.
Ziara ya TISEZA katika mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji wa uwekezaji wa ndani, inayoendelea katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, kwa lengo la kuhamasisha Watanzania kuwekeza katika miradi ya kimkakati inayochangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi.






No comments: