LIVE STREAM ADS

Header Ads

SEHEMU YA KWANZA: TARIME ZIPO MILA ZA KUKUMBATIA, LAKINI SI UKEKETAJI.



Wasichana Wakikeketwa
Ni miaka mingi sasa, tangu mila ya ukeketaji ianze kutekelezwa katika nchi mbalimbali hapa duniani, Afrika Mashariki na hata Tanzania, ambapo bado juhudi za kutokomeza Mila hiyo zinazofanywa na wadau mbalimbali, yakiwemo mashirika na taasisi za serikali na binafsi hazijaweza kuzaa matunda.


Nchini Tanzania katika Mkoa wa Mara, Mila hii imekuwa ikitekelezwa na kabila la wakurya kwa kiasi kikubwa tangu enzi za mababu na mabibi zetu, huku jambo la kusikitisha likiwa ni kwamba bado mila hiyo inaendelea kukumbatiwa na watu wa  kabila hilo.


Pamoja na madhara ya wazi kabisa yanayotokana na ukeketaji kwa wasichana, bado idadi kubwa ya watu wa kabila la wakurya wakiwemo wazee wa kimila Wilani Tarime wanaamini ya kwamba ukeketaji hauna madhara yoyote kwa wasichana.


Lakini ukweli ni kwamba kuna madhara mengi yanayotokana na ukeketaji kwa wasichana, madhara ambayo ni pamoja na binti kupoteza damu nyingi wakati na baada ya ukeketaji, kupata madhara ya kiafya ikiwemo wakati wa kujifungua na wakati mwingine kupoteza maisha sanjari na kupata maumivu makali wakati wa ukeketaji na mengine mengi.


Makala hii imejikita tu katika Wilaya ya Tarime ambayo kwa mjibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Wilaya ya hiyo ina wakazi Laki Tatu, Elfu thelathini na tisa, Mia sita tisini na tatu (339,693) ambapo kati ya hao wanawake ni Laki Moja, Elfu sabini na sita, Mia saba na saba (176,707)  wakati Wanaume wakiwa Laki moja elfu sitini na mbili, Mia tisa themanini na sita (162,986).


Katika takwimu hizo jambo la kusikitisha ni kwamba idadi ya mabinti wanaofanyiwa ukeketaji bado ni kubwa Wilayani Tarime, ambapo inakadiliwa kwamba kwa koo moja ya kabila la Wakurya zaidi ya wasichana elfu Tatu hufanyiwa ukeketaji kwa msimu mmoja, ambapo zoezi hilo hufanyika mara moja kwa mwaka, kila baada ya mwaka mmoja.


Baadhi ya wananchi Wilayani Tarime wanaeleza kwamba pamoja na mwitikio wa utekelezaji wa mila hii kuanza kupungua japo kwa kiasi kidogo sana kwa baadhi ya maeneo Wilayani humo kutokana na juhudi za mashirika na taasisi mbalimbali kuanza kutoa elimu ya kupambana na ukeketaji, bado elimu hiyo haijawafikia vyema watu wote hususani wazee wa kimila na mangariba, na hivyo kuna haja ya jambo hilo kutiliwa mkazo zaidi.

MTANZANIA MEDIA: ITAENDELEA...

No comments:

Powered by Blogger.