SEHEMU YA TATU: TARIME ZIPO MILA ZA KUKUMBATIA, LAKINI SI UKEKETAJI.
![]() |
Wasichana Wakikeketwa |
Mfano ni
Ghati Chacha na Bhoke Chacha (Si majina yao halisi) ambao ni ndugu wote wakiwa
ni wahimu wa kidato cha nne mwaka jana katika shule ya Sekondari Rebu iliyoko
Wilayani Tarime, wanaeleza kwamba katika msimu wa ukeketaji wa mwaka 2012
walikumbana na changamoto ya kulazimishwa kwenda kukeketwa lakini waliweza
kukataa haswa kutokana na elimu ya madhara ya ukeketaji waliyokuwa wameipata
shuleni sanjari na kushuhudia namna dada yao alivyotokwa na damu nyingi pindi
alipokeketwa.
“Kwa mfano
mimi nililazimishwa kwenda kukeketwa lakini nilikataa, nilipoona wanazidi
kunilazimisha ilibidi nikimbie nyumbani hadi msimu wa ukeketaji ulipoisha ndipo
nikarudi nyumbani; hivyo nawashauri mabinti wenzangu ni bora mtu ukimbie
nyumbani kuliko kukubali kwenda kukeketwa” alisema mmoja wa mabinti hao.
Wazee wa
kimila nao bado wanahitaji elimu ya kutosha ili kuweza kutokomeza suala hili la
ukeketaji, kwa kuwa wao wanadai kila kabila lina mila yao na hiyo ni mila
iliyokuwepo tangu enzi na enzi na haina madhara yoyote katika jamii, kama
alivyoeleza mojawapo wa wazee wa kimila kutoka katika koo ya Watimbaru katika
kabila la wakurya Wilayani Tarime aliejitambulisha kwa jina la Mwikwabe Mwita
Masero.
“Hii mila
ilikuwepo tangu zamani; hivyo kama ni kuisha itaisha yenyewe lakini sisi
hatuwezi kuizuia kwa kuwa kufanya hivyo tutakuwa tunaingilia mamlaka ya akina
mama (Mangariba) na wataona kama tumeipindua serikali yao; japo hatukatai mila
hii kutokomezwa lakini ni vyema tukaacha hadi itakapoisha yenyewe” alisema mzee
huyo na kuongeza;
“Serikali
ndiyo inayozuia ukeketaji lakini sisi hatuoni madhara yake kwani hata mabibi
zetu walikeketwa na hawakupata madhara yoyote; hivyo kama ni madhara labda awe
nayo mtu mwenyewe lakini sisi hatuwezi kumsababishia mtu madhara kwa kumkeketa”
alisema Mzee Masero tena kwa umakini mkubwa.
Mzee huyo
alihitimisha kwa kusema kuwa katika msimu wa ukeketaji ambao hufanyika mara
moja kwa mwaka, kila baada ya miaka miwili, idadi ya wasichana wanaofanyiwa
ukeketaji inakadiriwa kufikia kati ya elfu tatu hadi elfu nne kwa koo moja,
akiitolea mfano koo ya watimbaru.
“Idadi,
aaaah mfano katika koo ya watimbaru wanaweza kufika kama elfu tatu au elfu nne
hivi kwa msimu,” alisema mzee huyo tena bila mshangao wowote kulingana na idadi
hiyo jinsi ilivyokubwa.
MTANZANIA MEDIA: ITAENDELEA...
No comments: