LIVE STREAM ADS

Header Ads

CHONDE CHONDE VITA ZA KIKOO ZISIJIRUDIE TENA WILAYANI TARIME, MKOANI MARA.


Makala hii haina nia ya kukukumbusha aina yoyote ya vita zilizowahi kujili barani Afrika, bali inakukumbusha Vita za koo kwa koo katika kabila la Wakurya wanaopatikana Wilaya ya Tarime Mkoani Mara hapa nchini Tanzania.

Kabila la Wakurya ni kabila linaloundwa na koo 13 ambazo kwa ukaribu zinafanana kabisa katika Mila, desturi  na Tamaduni , zikiwa ni koo ambazo zilipatikana kutokana na mwasisi wa kabila hili kuwa na watoto 13 ambao baada ya kukua kila mmoja alianzisha familia yake ambayo mwishowe iliongezeka  na kuunda koo yake.

Jambo la kusikitisha koo hizi zilijikuta zinaingia katika vita, huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni migogoro ya ardhi na mipaka, sanjari na wizi wa mifugo baina ya koo hizi, ambazo miongoni mwake ni pamojan na koo ya Watimbaru, Warenchoka, Wanchari, Wakira, Wanyabasi, Wairege na nyinginezo zilizosalia.

Mwaka 2008 ilizuka vita ya koo kwa koo katika kabila la Wakurya baina ya Wanchari na Warenchoka, mwaka huo huo tena Wanchari wakapigana na Wakira,  huku mwaka 2009 Wanyabasi na Wairege wakiingia vitani, ambapo haikuishia hapo kwani mwa huo huo ,Wamera walipigana na Wahunyaga huku Wahunyaga wakipigana tena na Wasweta, ambapo utaona namna vita hiyo ilivyopamba moto kwani koo moja iliweza kuingia vitani na koo zaidi ya moja ndani ya mwaka mmoja.

Mapigano hayo yalisababisha athari kubwa katika  jamii kwa kuwa wananchi wasiokuwa na hatia waliweza kupoteza maisha, huku wengine wakipata ulemavu wa kudumu sambamba na wengine nyumba na mashamba yao vikichomwa moto sanjari na mazao yao kuharibiwa vibaya, hali ambayo ilirudisha nyuma maendeleo ya wananchi Wilayani Tarime.

Mpenzi msomaji nikiwa nimejikita katika Wilaya ya Tarime, nilizungumza na wananchi wa Wilaya hiyo ambao walikuwa mwenyeji wangu huko Tarime, ambao awali ya yote walinijuza kuwa vita hii ya koo kwa koo katika kabila la Wakurya huwa likuwa ikisababishwa na sababu kuu mbili ambazo ni wizi wa mifugo na migogoro ya ardhi baina ya koo na koo.

“Eee suala la wizi wa mifugo linachangia sana kusababisha vita hii, unakuta koo Fulani kwa mfano watimbaru wanaweza kuwa wameibiwa mifugo yao ikawa imeelekea sehemu ya wakira, sasa wale wafatiriaji wanapofika sehemu ya wakira, wanapojaribu kuhojiana ili wawasaidie kupata mifugo na ikashindikisha basi vita baina ya koo moja na nyingine huanzia hapo” alisema mmoja wa wananchi hao.

Sisi sote ni mashahidi ya kwamba hakuna vita iliyo ndogo wala kubwa katika jamii, na pale inapoibuka vita katika eneo lolote lile ni lazima madhara yapatikane, na hiyo ndiyo sababu iliyonilazimu kutaka kufahamu madhara ya vita hii ya koo kwa koo Wilayani Tarime.

“Vita kama vita ina madhara, kwanza mnapoteza muda wenu mwingi mkiwa mnapigana mnashindwa kufanya shughuli zenu za kilimo kwa hiyo mnaleta njaa, pili kuna maana yanapatikana kwa maana ya mauaji…”alieleza mwananchi mwingine.

Ni ukweli usiopingika kwamba ili vita iweze kupamba moto kunahitajika kuwepo na silaha kwa ajili ya mapambano na kujihami, sasa kwa wenzetu Wakurya silaha zilizokuwa zikitumika katika vita baina ya koo na koo Wilayani Tarime ni za jadi kama vile mapanga, mikuki, mishale na kwa silimia chache silaha za kisasa kama vile bunduki.

Itakumbukwa kwamba baada ya vita hii kupamba moto, serikali iliamua kuanzisha Mkoa wa Kipolisi wa Tarime na Rorya kwa lengo la kufikisha karibu huduma ya ulinzi na usalama kwa wananchi, hatua ambayo inapongezwa na wakazi wa Tarime kwa kuwa imesaidia kupunguza machafuko Wilayani humo.

“Kwanza nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali yetu kwa kutuletea kikosi maalumu cha polisi Wilaya ya Tarime na Rorya, kimetusaidia san asana kupunguza hii tabia ya vita, kwanza imepunguza wizi wa mifugo na hata ulimaji wa bangi katika Wilaya yetu kwa hiyo naishukuru sana Serikali hii ya Kikwete…”Alieleza mwananchi wa Kijiji cha Kenyamanyori niliezungmza nae.

Ni ukweli usiopingika kwamba hakuna mtu hata mmoja anaependa kushuhudia vita ikitokea katika eneo lake, kwa suala la umwagaji wa damu nao huchukua nafasi yake katika maeneo ya vita, kutokana na hilo mwenyeji wetu anasema elimu itolewe kwa wananchi ili kuachana na migogoro ya ardhi na wizi wa mifugo ambavyo vilikuwa vikisababisha vita za mara kwa mara Wilayani Tarime.

Kuna kipindi wazee wa kimila nao waliweza kutupiwa lawama kuwa wanachochea vita hii ya koo kwa koo katika kabila la Wakurya, lakini kwa hivi sasa hali iko tofauti kwa kuwa wazee hao wote kutoka katika koo zote 13 wameungana pamoja lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa vita hiyo inatokomezwa kabisa.

Mzee mmoja ambae ni miongoni mwa wazee wa kimila kutoka katika koo ya Watimbaru, anafafanua kwamba wao kama wazee walikuwa hawafurahishwi na vita za mara kwa mara baina ya koo na koo katika maeneo yao kwa kuwa zilikuwa inaleta chuki miongoni mwa wanajamii.

Kwa sasa vita Wilayani Tarime imesitishwa japo sina jibu la moja kwa moja kama vita hii ni kweli imefikia kikomo kwa kuwa vita hii huwa ni ya msimu, hivyo ni matumaini yangu kuwa Wakurya wataweza kutumia fursa hii kuweza kukaa pamoja na kusitisha vita hiyo haraka iwezekanavyo, lakini elimu ndiyo njia pekee ambayo inapendekezwa na wengi kutumika ili kuweza kuendelea suala la amani miongoni mwa wananchi wa Wilaya ya Tarime.

Lakini kwa mjibu wa mzee wetu wa kimila kutoka Wilayani Tarime ni kwamba vita hiyo kwa hivi sasa haipo na koo zote zinaishi kwa amani, kwa kuwa vita hiyo ikionyesha dalili ya kuibuka wazee wote wa kimila hukaa katika eneo lenye mgogoro na vita hiyo husitishwa mara moja.

Pia mzee huyu anasema kwamba suala la matambiko pia limekuwa likisaidia sana katika kuhakikisha amani na usalama inakuwepo katika jamii, ambapo anaeleza kwamba hata katika vita hii ya koko kwa koo katika kabila la Wakurya Matambiko yamesaidia kuleta utulivu wa amani.

“Matambiko yanasaidia sana kuleta amani kwenye koo, huwa tukitaka kufanya matambiko ya amani huwa tunaitaarifu serikali na tunafanya matambiko yetu kwa amani ambapo mnyama huchinywa na watu hula na kunywa tunapokuwa tunafanya matambiko yetu katika kipindi Fulani, mfano wakati wa njaa ama vita” Alisema mzee huyo wa Kimira.  

Japo nilitamani sana kusikia kutoka kwa upande wa jeshi la polisi, kanda maalumu ya Tarime na Rorya lakini hadi naondoka Wilayani humo sikuweza kufanikiwa. Lakini naamini kwa hayo machache niliyoyapata kutoka kwa wananchi wa Tarime wametupatia mwanga kidogo juu ya vita za koo katika kabila la Wakura Wilayani Tarime.
Maoni/ Ushauri 0757 43 26 94

No comments:

Powered by Blogger.