WANAFUNZI WA DARASA LA SITA, SHULE YA MSINGI NYANZA MKOANI MWANZA WAFANYA MAAJABU MAKUBWA.
![]() |
Mkuu wa Shule ya Msingi Nyanza Mwl.Ulinyelusya Tumbo ambae pia ni mwalimu wa Somo la Stadi za Kazi akiwafundisha wanafunzi wa darasa la Sita shuleni hapo. |
![]() |
Ni wanafunzi 10 kati ya 40 wa darasa la Sita wanaosoma Shule ya Msingi Nyanza Iliyoko Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza, wameweza kuitumia likizo hii ya mwezi wa Sita vyema kwa kuweza kukaa na mwalimu wao anaewafundisha somo la Stadi za kazi na kupata mafunzo ya ushonaji wa Vikapu.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya hiyo Mwalimu Ulinyelusya Tumbo ambae pia ndie Mwalimu anaewafundisha somo la Stadi za Kazi amebainisha kuwa, wanafunzi hao alianza kuwafundisha somo hilo tangu mwaka jana wakiwa darasa la tano na wamekuwa wakijifunza kutengeneza vitu mbalimbali vinavyohusiana na kazi za mikono kama sehemu yao ya kujinza.
"Tulivyoanza kila mwanafunzi aliandika kitu anachopenda kukifanya, kuna walioandika mapambo, ufinyanzi, ususi, uchoraji na hiyo kazi tuliifanya mwaka mzima toka mwaka jana, hatimae walianza kutengeneza vitu kama chen (mikufu), mipira na kuviuza..."Alisema mwalimu Tumbo.
Aidha alibainisha kuwa baada ya kuwa wanafunzi hao wameanza kuvutiwa na bidhaa wanazozitengeneza, aliamua kuwashirikisha katika wazo la kujifunza na kutengeneza vikapu katika kipindi hiki cha likizo, ambapo aliwaomba kuchangia pesa kidogo kwa ajili ya kumuwezesha atakaekuwa anawafundisha.
"Niliwashirikisha waweze kuchangia kidogo ili katika kipindi hiki cha likizo waweze kuwa na muda mwingi wa kujifunza kutengeneza vikapu, nasikitika kwamba waliojitokeza ni wanafunzi 10 pekee kati ya wanafunzi 40, ambao hawakushiriki nilipowauliza walisema wazazi wameshindwa kuwapa pesa kwa ajili ya kumlipa atakae kuwa anawafundisha, ndo uone sasa jinsi gani wazazi hawataki wanafunzi wao wajifunze kazi za mikono ambapo zinaweza kuwasaidia kuongeza kipato hata wakiwa na kazi za ofisini"
Wanafunzi wanaopata mafunzo hayo ya kutengeneza vikapu wanasema kuwa wanayafurahia mafunzo wanayoyapata na wanatarajia mabadiliko makubwa hapo baadae kwa kutengeneza vitu vizuri zaidi kutokana na kazi za mikono ikiwa ni pamoja na mikufu na vikapu huku wakibainisha kuwa kazi za mikono zina maana kubwa katika kujiongezea kipato hata kama utakuwa umeajiriwa.
Shaban Rajab pamoja na Magdalena Peter ambao ni wakufunzi katika mafunzo hayo, kwa pamoja wanasema kuwa kazi za mikono zina faida kubwa lakini wazazi hawajauona umuhimu uliopo kwa watoto wao, na hivyo kuwasihi wazazi na waalimu kuwajengea uwezo wanafunzi kujifunza kazi za mikono huku wakiisihi serikali kuongeza waalimu wa somo la Stadi za Kazi Mashuleni ili kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi unaotokana kazi za mikono.
No comments: