LIVE STREAM ADS

Header Ads

AICT DAYOSISI YA GEITA KUANZA KUTOA HUDUMA ZA AFYA ZIWA VICTORIA KWA KUTUMIA MELI.

Meli ya MV. Jubilee Hope inayotarajiwa kufanya shughuli za kutoa huduma za Kiafya kwa wananchi na wakazi wanaoishi katika Visiwa vya Ziwa Victoria ikiwa ni katika Mikoa Mitatu ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Geita na Kagera.

Kanisa la AICT Dayosisi ya Geita kwa Kushirikiana na Shirika la Vine Trust la Scotland inchini Uingereza linatarajia kuanza kutekeleza Mradi wa Kutoa huduma za Kimatibabu katika Visiwa mbalimbali ndani ya Ziwa Vikitoria.

Mradi huo ambao
unajulikana kwa jina la The Jubilee Hope Medical & Dental Programme umelenga kutoa huduma za Afya katika Visiwa vya Ziwa Victoria vinavyopatikana katika Mikoa Mitatu ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Geita, Kagera na Mwanza.
Kamati ya Uzinduzi wa Meli ya MV, Jubilee Hope ikiongozwa na Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Geita Askofu Mussa Magwesela (Wa tatu kutoka pande zote.)

Akitoa taarifa hii leo Mkoani Mwanza juu ya Mradi huo, Askofu wa Dayosisi ya Geita Mussa Magwesela alieleza kwamba Mradi huo unatarajia kutoa huduma mbalimbali za kimatibabu ambazo ni pamoja na Matibabu ya Meno, Matibabu ya Mtoto, Mama na Uzazi sanjari na kutoa elimu na huduma kwa watu waishio na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Aidha alibainisha kwamba mradi huo umekusudia kutekeleza shughuli zake kwa Mfumo wa Meli ya Matibabu ambayo itakuwa ikizunguka katika Visiwa vya Ziwa Victoria na kutoa huduma za Afya na Matibabu kwa wananchi wa Visiwa hivyo.
Mathias Ndetto (Kushoto) akiwa na Rev.Malobo Tungalaza (Kulia). Wote ni Wanakamati ya Uzinduzi wa Meli hiyo ya MV.Jubilee Hope.

Alisema kuwa Meli hiyo imepewa jina la MV. Jubilee Hope na inatarajiwa kuwasili katika Bandari ya Mwanza Kaskazini Kati ya Septemba 22 na 23 mwaka huu ambayo itakuwa ni Ijumaa ya wiki hii ikitokea Kisumu nchini Kenya, huku ikitarajiwa kuzinduliwa rasmi Septemba 27 mwaka huu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Jakaya Mrisho Kikwete katika Bandari hiyo ya Mwanza Kaskazini.

Hadi kukamilika kwa Mradi huo, zaidi ya Shilingi Bilioni Mbili zinatarijiwa kutumika huku uendeshaji wake kwa Mwaka ukikadiriwa kufikia Shilingi Milioni Mia Tano kwa Mwaka ambapo mafanikio ya Mradi huo yanatarajiwa kukamilika kwa ushirikiano wa karibu kabisa miongoni mwa Kanisa hilo la AICT Dayosisi ya Geita na Shirika la Vine Trust la Scotland inchini Uingereza ambalo limekuwa likifadhiri Miradi tofauti tofauti katika nchi mbalimbali duniani.
Dr. Ngallaba Sospatro (Kushoto) akiwa na Mrs.Pendo Limbe (Kulia). Wote ni wajumbe wa Kamati ya Uzinduzi wa Meli ya MV.Jubilee Hope.

Aidha Askofu Magwesela aliielezea Meli hiyo kuwa itakuwa na vyumba vitatu kwa ajili ya Madaktari kuwahudumia wagonjwa, Vifaa mbalimbali vya tiba, duka la Madawa baridi, Maabara kwa ajili ya Vipimo pamoja na eneo lenye uwezo wa kubeba watu kati ya 30 na 50 kwa ajili ya wagonjwa kusubiria kuonana na daktari.
Joseph Kahungwa ambae  ni Mjumbe Kamati ya Uzinduzi Meli ya MV.Jubilee Hope inayotarajiwa kuanza kutoa huduma za Kiafya kwa wananchi wanaoishi katika Visiwa vilivyoko Ziwa Victoria ikihudumu katika Mikoa Mitatu ya Mwanza, Geita na Kagera.
Askofu wa Dayosisi ya Geita Askofu Mussa Magwesela
Wanahabari.
Wanahabari katika Kunasa Habari.

No comments:

Powered by Blogger.