LIVE STREAM ADS

Header Ads

MAMLAKA YA USIMAMIZI WA SEKTA YA HIFADHI YA JAMII SSRA YASHIRIKI MAONYESHO YA MWANAMKE NA UCHUMI MKOANI MWANZA.

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza Amina Masenza (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Neema Malima Mkurugenzi wa Taasisi ya Angels Moment (wa kwanza kushoto), anaefuata ni Sarah Kibonde Msika Afisa Mawasiliano, Promosheni na Uhamasishaji kutoka SSRA na wa Mwisho kulia ni Mama Ndikilo (Mke wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Evarist Ndikilo)
Mkurugenzi wa Kampuni ya Mafuta ya MOIL Altaf Mansoor (Kulia) akiangalia Majarida katika banda la Mamlaka ya Mfuko wa udhibiti Mifuko ya Hifadhi za Jamii nchini (SSRA). Kushoto ni Sarah Kibonde Msika ambae ni Afisa Mawasiliano, Promosheni na Uhamasishaji kutoka SSRA.
Neema Malima Mkurugenzi wa Taasisi ya Angels Moment (katikati) akiwa na baadhi ya watumishi wa Taasisi hiyo.

Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii nchini (SSRA) imeshiriki katika Maonyesho ya Siku mbili ya Mwanamke na Uchumi yaliyofanyika Mkoani Mwanza, ambapo Wananchi wamepata fursa ya kuelimishwa masuala mbalimbali kuhusiana na Mamlaka hiyo sanjari na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa Ujmla.

Mamlaka hiyo imeshiriki Maonyesho hayo ambayo yalifanyika wiki hii kuanzia Septemba nne hadi Septemba tano mwaka huu, katika Uwanja wa Magomeni uliopo Kirumba Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza.
Katika banda la SSRA wananchi waliweza kupata ufafanuzi kuhusiana na jukumu kubwa la Mamlaka hiyo, ambalo ni kuhakikisha kuwa Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamiii inakuwa endelevu, Maslahi ya Wanachama yanalindwa, inaendeshwa kwa kufuata kanuni na taratibu za kisheria, wanachama kupata michango yao sanjari na mafao kuhakikisha kuwa yanaboreshwa.

Mbali na hayo, pia Mamlaka hiyo ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii SSRA ina dhima ya kuhakikisha kwamba huduma bora za Hifadhi ya Jamii zinamfikia kila Mtanzania kupitia usimamizi madhubuti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii.
Aidha kwa Mjibu wa Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi nz Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii, Mamlaka hiyo inafanya kila jitihada ili kuhakikisha kuwa inatimiza wajibu na majukumu yake ipasavyo.

Miongoni mwa wajibu na majukumu hayo ni pamoja na kuweka Mazingira mazuri ambayo yatapanua wigo wa Hifadhi ya Jamii na Kuongeza wanachama hususani walio katika Sekta zisizo rasmi sanjari na kutetea na kulinda Maslahi ya Wanachama.
Neema Malima Mkurugenzi wa Taasisi ya Angels Moment ambao ni waandaaji wa Kampeni ya Mwanamke na Uchumi iliyofanyika Mkoani Mwanza Septemba 04 hadi 05 mwaka huu akiwa katika banda la Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA).

Katika Maonyesho hayo, wananchi nao wakapata fursa ya kufahamu baadhi ya mambo yanayowahusu kuyatimiza wakiwa kama wafanyakazi kuwa ni pamoja na kujiunga na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa lengo la kunufaika na huduma mbalimbali za Hifadhi ya Jamii huku wale waliokwisha jiunga wakikumbushwa kufuatilia michango yao yote kama inawasilishwa katika mifuko waliyojiunga nayo.

Zaidi ya yote, Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ikatumia Maonyesho hayo kutoa wito kwa wananchi wote kutumia ipasavyo fursa zote zinazotolewa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Ambapo Mifuko hiyo ni Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Mafao ya Kustaafu (GEPF), Mfuko wa Pensheni wa (PPF), Mfuko wa Pensheni wa (LAPF), Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambapo kila mwananchi au mtumishi anayo fursa ya kuchagua mfuko anaopenda kujiunga nao.

Hifadhi ya Jamii inamuwezesha mwananchi kuishi maisha yenye staha kwa kumuwezesha kupata huduma za msingi pale hana kipato kutokana na sababu mbalimbali. Ambapo huduma hizo zinaweza kupatikana kupitia mafao mbalimbali kama vile mafao ya uzee, kifo, ugonjwa, uzazi n.k
Maonyesho hayo yaliambatana sambamba na Kampeni ya Mwanamke na Uchumi ambayo iliwahusisha zaidi ya Wanawake Wajasiriamali 1,000 kwa siku zote mbili kutoka Wilaya tatu za Mkoa wa Mwanza ambazo ni Magu, Nyamagana na Ilemela.

Wanawake hao Wajasiriamali walikutana chini ya Uratibu wa Taasisi ya Angels Moment ya Jijini Dar es salaam kwa lengo la kuwapata elimu ya Msingi juu ya Masuala mbalimbali ya Ujasiriamali ili kuziba changamoto zinazowakabili katika Masuala ya Ujasiriamali.
Wananchi wakipata ufafanuzi katika banda la Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA).
Mwandishi wa Habari wa Radio Kwizera (Kushoto) akimhoji Mama Mjasiriamali Katika Maonyesho ya Mwanamke na Uchumi Mkoani Mwanza.
Wanawake Wajasiriamali Mkoani Mwanza wakifuatilia somo kwa umakini katika Kampeni ya Mwanamke na Uchumi iliyoandaliwa na Taasisi ya Angels Moment kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto pamoja na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA). Baada ya Mwanza, Kampeni hiyo itaendelea katika Mikoa ya Kigoma, Tanga, Ruvuma, Dodoma, Pwana na Lindi ikitarajiwa kunufaika na Kampeni hiyo hapa nchini.
Na: George Binagi @99.4 Metro FM & Mtanzania Media.

No comments:

Powered by Blogger.