LIVE STREAM ADS

Header Ads

MACHINGA MKOA WA MWANZA WAGAWANYIKA MAKUNDI MAKUNDI. WAMTAKA MKUU WA MKOA KUINGILIA KATI.

Viongozi wa Jumuiya ya Wafanyara ndogondogo katika Masoko na Minada Mwanza ambapo Kushoto ni Amos Thomas (Mtunza Hazina), katikati ni Justine Sagara (Mwenyekiti) na Kulia ni David Philipo (Katibu).
Baada ya jana Muungano wa Machinga Mkoa wa Mwanza kufanya Uchaguzi Mkuu, Jumuiya ya Wafanyabiashara ndogondogo katika Masoko na Minada Wilaya za Ilemela na Nyamagana Mkoani Mwanza imeibuka na kutoa malalamiko yake kutokana na Uchaguzi huo.


Malalamiko ya Jumuiya hiyo yameibuka kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni Muungano wa Machinga Mkoa wa Mwanza kufanya Uchaguzi wa kuwapata viongozi watakaokuwa wanawasimamia Machinga wote Mkoa wa Mwanza, wakati katika Mkoa wa Mwanza Machinga wamegawanyika katika Makundi mbalimbali ambayo tayari yana Umoja na Uongozi wake.

Hayo yalielezwa jana na
Justine Sagara ambae ni Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo ya Wafanyabiashara ndogondogo katika Masoko na Minada kutoka Wilaya za Ilemela na Nyamagana wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ofisi za Jumuiya hiyo zilizopo Kiloleli Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza.

Sagara alibainisha kwamba wanaosema Uchaguzi wa Muungano wa Machinga Mkoa wa Mwanza uliofanyika jana unajumuisha Machinga wote wa Mkoa wa Mwanza, wanaupotosha Umma kwa kuwa Uchaguzi huo haukuyajumuisha Makundi yote ya Machinga Mkoa wa Mwanza.

Kutokana na hali hiyo Sagara alimuomba Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Magesa Mlongo kukutana na Makundi yote ya Machinga Mkoani Mwanza ili kutafuta namna ya kuweza kuyaunganisha Makundi hayo kwa lengo la Kupata uongozi mmoja wa Kuweza kuwasemea Machinga.

Katika hatua nyingine Sagara alibainisha kwamba kwa muda Mrefu Jumuiya ya Wafanyabiashara ndogondogo katika Masoko na Minada imekuwa ikishirikiana na vyema na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, lakini Jumuiya hiyo imekuwa ikikosa Ushirikiano kutoka katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza, licha ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza kukusanya Ushuru katika Masoko na Minada ambayo Jumuiya hiyo imekuwa ikifanyia biashara zake.

Kutokana na suala hilo, Sagara alisema kuwa Jumuiya hiyo ya Wafanyabiashara ndogondogo katika Masoko na Minada Wilaya za Ilemela na Nyamagana imetishia kuwa Kuanzia jumatatu ijayo ya Januari 26, 2015 haitakuwa tayari kulipia Ushuru katika Minada iliyopo katika Wilaya ya Nyamagana ambayo ni Mkuyuni, Machinjioni Voil, Mkolani, Igoma na Mirongo hadi pale Halmashauri ya Jiji la Mwanza (Nyamagana) itakapotambua uwepo wa Jumuiya hiyo.

Machinga Mkoa wa Mwanza wamegawanyika katika Makundi mbalimbali ambayo kila moja linaunda Uongozi wake ambapo Makundi hayo ni pamoja na Shirika la Umoja wa Machinga Tanzania SHIUMA TZ, Muungano wa Machinga Mkoa wa Mwanza pamoja na Umoja wa Wafanyabiashara ndogo ndogo katika Masoko na Minada kutoka Wilaya za Ilemela na Nyamagana.

Nje ya Jumuiya hiyo ya Umoja wa Wafanyabiashara ndogondogo katika Masoko na Minada Mwanza, katika Uchaguzi uliofanyika katika kwa ajili ya kuwapata Viongozi wa Muungano wa Machinga Mkoa wa Mwanza, Viongozi waliochaguliwa ni Jamal Said ambae ni Mweka Hazina kwa Kura 881, Katibu Mwenezi Athuman Juma kwa Kura 767, Katibu Msaidizi David Juma aliepita bila kupingwa, Katibu Mkuu akiwa ni Moshi Maketa aliepata Kura 700, Makamu Mwenyekiti ni Tatu Festo na Mwenyekiti ambae ni Said Athuman Tembo ambae alichaguliwa kwa Kura 819.

Uchaguzi huo ulifanyika jana January 21, 2015 katika Uwanja wa CCM Kirumba kufuatia Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo kuuagiza Muungano huo wa Machinga Mkoa wa Mwanza kufanya Uchaguzi wake kufuatia malalamiko yaliyotolewa na baadhi ya Machinga kuwa Umoja huo kwa Muda mrefu haukuwa na Uongozi unaoeleweka.

MSIKILIZE HAPA CHINI SAGARA AMBAE NI MWENYEKITI WA JUMUIYA YA WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO KATIKA MASOKO NA MINADA MWANZA.

Viwaro katika Mnada wa Kiloleli Ilemela Mkoani Mwanza.
Suti za Kutosha katika Mnada wa Kiloleli Ilemela Mkoani Mwanza.
Na hizi pia huwa zinapatikana Kiloleli Ilemela Mkoani Mwanza.
Manunuzi katika Mnada wa Kiloleli Ilemela yakiendelea.
Huu ndio Umoja wetu.
Na: George Binagi-GB Pazzo.

No comments:

Powered by Blogger.