LIVE STREAM ADS

Header Ads

MACHINGA NA MADEREVA WA MAGARI YA MIZIGO WAZUA TAHARUKI JIJINI MWANZA.

Wafanyabiashara ndogondogo maarufu kwa jina la Machinga Jijini Mwanza wamezua taharuki hii leo asubuhi, baada ya kuingia katika Mzozo na Madereva wa Magari ya Mizigo wanaopaki magari yao katika eneo la Stand ya Zamani Maarufu kama Nyanganyika Bus.

Taharuki hiyo imeibuka baada ya baadhi ya
Machinga kwa Kushirikiana na Viongozi wao wapya waliochaguliwa Juzi kupitia Uongozi wa Muungano wa Machinga Mkoani Mwanza kufika katika eneo hilo la Tanganyika basi na kuanza kujigawia maeneo ya ajili ya kufanyia biashara kwa minajiri kwamba eneo hilo ni lao hivyo Magari hayo ya Mizigo (Malori) yanapaswa kuondoka katika eneo hilo.

Kutokana na hali hiyo, hatimae Madereva wa Malori waliamua kuondoka katika eneo hilo la Tanganyika Bus na kwenda kuegesha Malori yao ambao yalikuwa zaidi ya 100 katika barabara ya Pamba jambo ambalo lilizidi kuzua usumbufu zaidi kwa kuwa barabara hiyo pia inatumiwa na Magari ya abiria maarufu kama daladala.

Hadi tunakwenda Mitamboni, Mwenyekiti wa Uongozi Mpya wa Muungano wa Machinga Mkoa wa Mwanza alikuwa katika Kikao cha pamoja baina yake na Viongozi wengine ambao hakuwataja majina kwa ajili ya kutafuta suluhu la suala hilo ambapo ameahidi kuzungumza nasi baada ya Kikao hicho kumalizika.

Alipotafutwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Halifa Hida alibainisha kwamba hayuko katika hali nzuri kiafya hivyo hawezi kulizungumzia suala hilo kwa sasa.

Taharuki ya Machinga hao hii leo ilifikia pabaya baada ya baadhi ya Machinga na Madereva hao wa Malori kuanza kujitokeza huku wakiwa na silaha za jadi kama vile mapanga hali ambayo ilionekana kutishia usalama kwa wanainchi na mali zao.

Juhudi za Kumtafuta Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza ili kuzungumzia taharuki hiyo bado zinaendelea, japo hadi tunatoka katika eneo la tukio hakukuwa na afisa yeyote wa polisi aliekuwa amefika katika eneo hilo kwa ajili ya kutuliza hali iliyokuwa imejitokeza.
Na: Mwandishi Wetu-Mtanzaniamedia Blog

No comments:

Powered by Blogger.