LIVE STREAM ADS

Header Ads

MAKALA: NYUMBA ZA UTIMAMU WA MWILI ZINASAIDIA WATEJA KUACHA DAWA ZA KULEVYA.

Na: Edwin Soko.
Uwepo wa   nyumba  za  utimamu wa mwili     kwa  watumiji wa  dawa za kulevya  Nchini,  umesaidia  kupunguza  tatizo  la dawa  za kulevya  kwa  baadhi  wa  watumiaji  waliojitambua  na kuwa  tayari  kuacha  dawa   hizo  kwa  kupata  programu  maalumu  zenye  ushawishi wa    kujitambua  na kuwa   huru  bila  kutumia  dawa za kulevya .

Vituo  hivyo  maarufu  kama   Nyumba za utimamu wa mwili   (rehabilitation  centres  au  sober  houses)  zimekuwa  vikitambulika  na  serikali  na kufanya  kazi  chini  ya  miongozo  ya    serikali.  Nchini   Tanzania  vituo  hivi vinapatikana  katika  mikoa  mbalimbali ikiwemo, Tanga, Dar es Salaam, Zanzibar , Arusha  na Mwanza, huku vikiwa  na  msaada mkubwa  kwa  watumiaji wa dawa za kulevya .

Nilitembelea  moja  ya  kituo   hicho  kinachojulikana  kwa  jina la 
Pili Misanah  kilichopo   Pasiansi, Wilaya  ya  Ilemela  Jijini Mwanza  na kukutana  na meneja   wa kituo  hicho,   bwana  Mohammed  Mohammed, ambaye  aliniambia    shughuli  zinazofanywa  na  kituo  hicho,  zikiwemo  kuwahamasisha  watumiaji wa  dawa  za kulevya  kuhudhuria  mafunzo   ya  kuacha  kutumia  dawa  za kulevya, kuwa  na moyo wa kujitambua   na kujikubali  kuwa  wao  ni watumiaji wa dawa za kulevya  na wanaweza kuishi   bila  kutumia  dawa za kulevya (Drug  free)  na kutambua  na kuvishinda    vishawishi  vya  dawa za kulevya.

Bwana  Mohammed  alisema  kuwa  mchango  wa  kituo  hicho  ni  mkubwa  sana katika  jamii, kwani  wateja  wengi   wamekuwa  wakiachana  na uteja  kwa kupata   mafunzo  ya  namna  ya  kuacha     dawa  za kulevya .

“Tulianza   kutoa  huduma  hizi   Februari, 2014  na   watu  zaidi  ya  sabini wamepata  huduma  hii  na  kati  ya hao    arobaini  wamepona  na kuacha  kabisa  kutumia  dawa za kulevya  na wanaendelea   vyema  na  shughuli  za kujenga  Nchi”, alisema   Mohammed.

Pia  alisema  kuwa   programu ya  kumbadili  mtu kutoka  kwenye  matumizi   ya  dawa za kulevya  na kuwa   msafi  (Drug   free),  inachukua  muda  wa miezi  sita kwa kufundishwa  juu  ya  kujikubali na kuwa  tayari  kuishi  nje  ya  maisha  ya  matumizi  ya  dawa za kulevya.

Naye   bwana  Emmanuel   Gofrey     aliyekuwa  mtumiaji  wa dawa  za kulevya  na sasa  amepona  kupitia   kituo  cha Pili   Missanah  alisema kuwa,    yeye  ameacha  kabisa  kutumia  dawa za kulevya  na kwa sasa  anafanya  biashara   ya  matunda  eneo  la  Kirumba  na anakishukuru  sana kituo  hicho  kwa kuwa  mkombozi wa watumiaji wa dawa za kulevya Jijini Mwanza.

Bwana  Lodrick  Ngowi, mkazi wa Mwanza   alisema  kuwa,  uwepo  wa   vituo  vya  kutoa  programu za  kuhamasisha  watu  kuacha  kutumia  dawa za kulevya  limesaidia   sana  kwani, yeye  kwa sasa anaishi  na  kijana  wake  ambaye  ameacha  kutumia dawa za kulevya  na amepona kabisa   baada  ya  kijana    huyo  kupelekwa  kwenye  kituo    hicho.

Makala  hii  pia  ilibaini  changamaoto  ya  uwepo wa uingiaji  kwenye  kituo  hicho   kwa waathirika  wa dawa za kulevya wanaotaka  huduma  ya  kuacha  dawa  za kulevya, kwa kukosa  pesa ya  kulipia  ambayo  ni  shilingi  laki  mbili. Kiwango  hicho  kimeonekana    kikubwa  na  hivyo  wanaoingia  kituoni hapo  ni  watu  wenye  uwezo na  wasio  na uwezo  basi  hawataweza kupata  huduma  hiyo.

Kwa  mujibu wa  Daktari  Kasian Nyandidi  wa  hospitali  ya  Muhimbili Jijini  Dar es Salaam, alisema kuwa,    baadhi  ya  wateja  wanaopata   huduma  kwenye  vituo   hivyo  wamekuwa     hawaachi  kabisa  matumizi  ya dawa za kulevya, kwani    baadhi  ya  tafiti  zilizowahi  kufanywa     kwa kuchukua  sampuli  za  haja  ndogo  na  kuzipima  majibu  yameonyesha  kuwa  bado wanatumia   dawa za kulevya  huku  wakijitangaza  kuwa  wameacha  kutumia  dawa  na kuwa  huru.

Nyandidi  aliongeza  kuwa  ni  vyema  kwa jamii  ikatumia  njia  zote    za kusaidia  watu  kuacha  kuwa  wateja  wa dawa za kulevya    tofauti  na kuamini  njia  moja  ambayo  inaweza kuwa  na majibu  tofauti, baadhi  ya  njia  zinazoweza   kutumia   ni   matumizi  ya  tiba  ya  methadone  ambayo  imeanza  kutolewa kwenye    hospitali  ya  Mwananyamala, Muhimbili  na  Temeke.


Yote  ya  yote  makala   hii  imebaini  kuwa    programu  zinazotolewa  katika   vituo     hivyo  zinaweza  kufanya  kazi  tu  endapo  mhusika  ataweza kujitambua  na kuwa  tayari  kubadilika  na  kuacha  dawa za kulevya, kwani  zinafundisha  zaidi  mtu  kujitambua na  kuwa  msafi  wa  kiroho, kifikra  na kimatendo  juu  ya  kuishi  huru  bila matumizi ya dawa  za kulevya. 

Kwa  ushauri wasiliana    na Mwandishi  wa makala  hii  kwa simu  0754551306
Makala  hii  imedhaminiwa  na   Mfuko  wa Kuvisaidia Vyombo  vya  Habari  Tanzania(TMF).

No comments:

Powered by Blogger.