SERIKALI KUFUTA ADA KWA SHULE ZA SEKONDARI HAPA NCHINI.
Serikali
imesema kuwa itahakikisha kwamba inaondoa ada kwa shule za Sekondari hapa
nchini ili kila mwanafunzi anaeanza darasa la kwanza aweze kupata fursa ya
kusoma hadi kufikia kidato cha nne.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Jakaya Mrisho Kikwete
aliyasema hayo hii leo, wakati akizindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya
mwaka 2014 katika hafla iliyofanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari
Majani ya Chai iliyopo Jijini Dar es Salaam.
Rais Kikwete alisema kuwa kupitia Sera hiyo, Serikali imeadhimia
kwamba suala la elimu ya kidato cha nne liwe suala la lazima kwa kila
mwanafunzi hivyo ili suala hilo liweze kufanikiwa Serikali imeona ni vyema
kuanzia mwakani ikaondoa ada kwa Shule za Sekondari zinazomilikiwa na Umma.
Alisema Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inatoa mwanzo na Matumaini
mapya katika Sekta ya Elimu hapa nchini ambapo ameongeza kuwa Sera hiyo ni nyenzo
mhimu kulipeleka Taifa katika Ukombozi ifikapo mwaka 2025.
Aidha alibainisha kwamba Sera hiyo imeadhimia kuwa kila mtoto anapaswa
kuanza darasa la awali kabla ya kuanza darasa la kwanza huku akibainisha kwamba
mwanafunzi ambae atamaliza darasa la saba bila kujua kusoma na kuandika
hataweza kuruhusiwa kuendelea na Masomo ya Sekondari.
Kuhusu Mkanganyiko wa Vitabu vya kufundishia mashuleni, Rais Kikwete
alisema kuwa yanahitajika mabadiliko ili kuhakikisha kwamba shule zote hapa
nchini zinakuwa na Vitabu vya aina moja (vyenye mtaala mmoja) ambavyo
vitatumika kufundishia katika Shule zote hapa nchini.
Aidha aliongeza kuwa Sera hiyo ya Elimu inalenga kutoa mwongozo wa
kupanga viwango vya ada kwa shule zinazomilikiwa na taasisi ama watu binafsi
badala ya kila shule kujipangia ada yake kadri inavyotaka jambo ambalo limekuwa
likilalamikiwa na wadau mbalimbali wa elimu.
Lakini pia Rais Kikwete aliwasihi waalimu kutambua umuhimu wao katika
kuleta mabadiliko chanya katika jamii na Taifa kwa ujumla ambapo amewataka
kutimiza wajibu wao ipasavyo kwa kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira
ya wao kufanyia kazi huku akitoa rai kwa wamiliki wa shule binafsi na wao
kutimiza ipasavyo wajibu wao na hivyo wajiepushe na kuifanya elimu kuwa
biashara.
Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 ambayo imezinduliwa rasmi hii leo na Rais
Kikwete imelenga kuboresha kiwango cha elimu hapa nchini ikiwa ni pamoja na
kuongeza miundominu ya elimu ikiwemo Maabara, Madarasa, Madawati pamoja na Waalimu.
Hafla hiyo ya Uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 pia
ilihudhuriwa na Waziri wa elimu na Mafunzo ya Ufundi Mh. Shukuru Kawambwa, Naibu
wake Kassim Majaliwa pamoja na Katibu Mkuu Wizara hiyo pamoja viongozi
mbalimbali wa Kitaifa na Kimataifa.
N: George Binagi-GB Pazzo
No comments: