LIVE STREAM ADS

Header Ads

TANZANIA BADO INATAFUNWA NA UINGIZAJI, USAFIRISHAJI NA MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA.

Katikati ni Edwin Soko ambae ni Mwenyekiti wa OJADACT akitoa taarifa kwa Vyombo vya Habari jana juu ya Maadhimisho ya Siku ya Kupiga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya Duniani yanayotarajiwa kufanyika Kesho. Kulia ni Neema Joseph ambae ni Mhasibu wa OJADACT na Kushoto ni Isaack Wakuganda ambae ni Afisa Jinsi OJADACT.
Na:George GB Pazzo
Wakati Tanzania leo ikiungana na Mataifa mbalimbali duniani Kuadhimisha Siku ya Kupiga Vita Matumizi ya dawa za Kulevya, imeelezwa kuwa bado Uingizaji, Usafirishaji na matumizi ya dawa hizo yako katika kiwango cha hali ya juu hapa nchini.

Hayo yalielezwa hii jana na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari wa kupiga vita matumizi ya dawa za Kulevya na Uharifu nchini OJADACT Edwin Soko, wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusiana na Maadhimisho hayo.

Soko alibainisha kuwa ripoti zinaeleza kwamba Tanzania ni kinara wa kupitisha dawa za kulevya katika nchi za afrika mashariki huku akibainisha kuwa katika Mkoa wa Tanga pekee katika kipindi cha kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka huu, ukamataji wa dawa za kulevya za aina mbalimbali uliongezeka kutoka kilo 145 hadi kilo 813.

Aidha Soko alibainisha kuwa Kumekuwa na uzembe wa makusudi kutokana na Serikali kushindwa kutaja nafasi ya Nchi kimataifa juu ya tatizo la dawa za kulevya na badala yake imekuwa ikificha uhalisia wa tatizo hilo ambalo amesema kuwa limekuwa kikwazo katika jamii kwani takwimu zinaonyesha kuwa katika Mkoa wa Mwanza pekee kuna zaidi ya Watumiaji wa dawa za kulevya za aina mbalimbali wapatao elfu Kumi ambapo Wilaya za Nyamagana na Ilemela zina watumiaji zadi ya Elfu tatu Mia tatu.

Kutokana na hali hiyo Soko alisema kuwa OJADACT inatoa rai kwa Serikali kwamba Vita   dhidi  ya  dawa  za kulevya  zinahitaji  nguvu  za pamoja ili  kukomesha biashara  hiyo pamoja na Serikali na  taasisi  mbalimbali kujikita katika  kutoa  elimu  ya  kutosha  juu  ya  dawa za kulevya.

Aliongeza kuwa Upatikanaji  wa  sera  ya  dawa  za kulevya  uharakishwe  ili  kusaidia  kumaliza  tatizo hilo pamoja na kuhakikisha kuwa Sheria  mpya  ya  dawa za kulevya  ya  mwaka 2014 inasimamiwa  na kutekelezwa  ipasavyo ili kuleta  tija kwa Taifa.

Mbali na hayo Soko alisema kuwa Vita  dhidi  ya  dawa za kulevya inapaswa kutangazwa kuwa ni janga  la kitaifa huku akisisitiza kuwa moja  ya  sifa  za Rais wa Tanzania  ajaye iwe ni kuwa  na  uwezo wa kukabiliana  na  biashara  ya  dawa za kulevya  kama  alivyofanya  Rais  Richard  Nickson  wa Marekani.

Kitaifa  Maadhimisho hayo yanafanyika  katika Wilaya Bagamoyo Mkoani Pwani ambapo katika Mkoa wa Mwanza yanafanyika Katika Kata ya Igogo Wilayani Nyamagana ambapo yanaambatana na Kaulimbiu isemayo "Jenga Jamii, Maisha na Utu bila Dawa za Kulevya".

No comments:

Powered by Blogger.