ZAHANATI YA MBUGANI JIJINI MWANZA YALALAMIKIWA.
Mmoja wa Wakazi wa Kata ya Mabatini akizungumza na GB Pazzo (Kulia).
Na:George GB Pazzo
Wananchi wa Kata Mpya ya Mabatini Jijini
Mwanza wameelezea kutoridhishwa na huduma za Afya zinatolewa katika Zahanati ya Kata hiyo iitwayo Zahanati ya Mbugani.
Baadhi ya Wananchi wa Kata hiyo ambayo
imegawanyika kutoka Kata ya Mbugani, waliyasema hayo wiki iliyopita wakati
wakizungumza na Radio Metro kupitia Kampeni yake ya Mtaa kwa Mtaa.
Walisema kuwa huduma za Afya katika Zahanati hiyo ambayo inahudumia Kata zote mbili za Mbugani na Mabatini
haziridhishi kutokana na uhaba wa vitendea kazi, dawa pamoja na Vipimo.
Aidha walilalamikia ukosefu wa
barabara inayopitika hadi katika zahanati hiyo ambayo imejengwa katika mwinuko,
kutokana na barabara inayoelekea katika zahanati hiyo kutopitisha magari,
pikipiki na hata baiskeli.
Afisa Mtendaji wa Serikali ya Mtaa wa
Mabatini Kusini ilipo Zahanati hiyo ya Mbugani alieleza kuwa bado hajapokea
malalamiko ya wananchi hao, japo hakuainisha ni changamoto gani lakini alikiri kuwepo baadhi ya changamoto katika Zahanati hiyo.
Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya
Zahanati hiyo alibainisha kuwa wahudumu wa Afya walio katika Zahanati hiyo
wanajitahidi kuwahudumia wananchi kadri ya uwezo wao, japo jitihada hizo zinakwamishwa na mapungufu yaliyopo ikiwemo ukosefu
wa vipimo na uhaba wa dawa.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu
wa Zahanati hiyo ya Mbugani, Esther Sonoko ambae ni Muuguzi alikiri Zahanati
hiyo kukabiliwa na changamoto kadhaa ambazo ni pamoja na ukosefu wa baadhi ya Vipimo
ambapo alisema kuwa kuna vipimo vya Malaria na HIV pekee, Uhaba wa dawa, Ukosefu wa
Kichomea taka (Insenereta) pamoja na ukosefu wodi ya akina mama.
No comments: